Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Washiriki watatu wa Tamasha la
Majimaji Selebuka lililofanyika mkoani Ruvuma wanatarajia kushiriki
mashindano ya Mbio za Baiskeli nchini Afrika Kusini Februari 19, 2017.
Hayo yamebainishwa leo na
Muandaaji Mkuu wa Majimaji Selebuka Reinafrida Rwezaura wakati wa
makabidhiano ya tiketi za ndege za kwenda Afrika Kusini kwa washindi hao
yaliyofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAEELEZO jijini Dar es
Salaam.
“Kikubwa kilichotukutanisha hapa
leo ni kuwaaga washindi wa Mbio za Baiskeli katika tamasha la Majimaji
Selebuka 2016, zilizofanyika tarehe 04 Juni 2016 kutoka Mbinga hadi
Songea umbali wa kilomita 100, ambao wanatakiwa kwenda kushiriki
mashindano ya Mbio za Baiskeli Jijini, Johanesburg, Afrika Kusini,”
alifafanua Rwezaura.
Rwezaura aliwataja washindi hao
wanaotegemea kwenda Afrika Kusini kuwa ni Salum Miraji ambaye alikuwa
mshindi wa kwanza , Allen Nyanginywa ambaye alikuwa mshindi wa pili na
Ipyana Mbogela ambaye alikuwa mshindi wa tatu.
Kwa upande wake, mshiriki wa
mashindano hayo Allen Nyanginywa ameishukuru Taasisi ya Songea
Mississippi (SO-MI) kwa kuandaa mashindano hayo pamoja na kutimiza ahadi
ya kuwasafirisha washindi wa kwanza hadi wa tatu kwenda nchini Afrika
Kusini.
Aliendelea kwa kusema kuwa
watahakikisha wanachukua ushindi nchini Afrika Kusini kwani huko
wanaenda kufanya kazi na wamefanya mashindano hayo ya Baiskeli imekuwa
ni kazi yao.
Majimaji Selebuka ni tamasha
linalofanyika kila mwaka mjini Songea, mkoani Ruvuma ambalo huandaliwa
na Taasisi ya Songea Mississippi (SO-Mi) ambapo kwa mwaka huu 2017
tamasha hilo linatarajia kufanyika kunzia Julai 23 hadi 30, 2017.
No comments:
Post a Comment