WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),
January Makamba amesema katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi na athari zake, ofisi yake imeandaa mradi utakaonufaisha shule
za msingi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Akiwa wilayani hapa, January alisema moja ya changamoto za Wilaya ya
Bagamoyo ni ukame unaotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi,
uliosababisha kupanda kwa kina cha bahari na kusababisha visima
vilivyochimbwa pembeni mwa miji na fukwe za bahari kufukiwa na maji na
chumvi.
“Ofisi ya Makamu ya Rais imeamua kuisaidia Wilaya ya Bagamoyo
kuchimba visima kumi na saba virefu kwenye maeneo ambayo yameathirika na
kupanda kwa kina cha maji na maeneo yenye ukame mkubwa,” alibainisha
January.
Takribani kila kisima kitagharimu Sh milioni 50 na Ofisi ya Makamu wa
Rais pia itaandaa mfumo wa kuvuna maji katika shule tano mradi utakao
gharimu takribani Sh milioni 170.
Katika hatua nyingine, alitembelea Kiwanda cha Sea Salt kilichopo
Saadani kuona namna kiwanda kinavyofanya kazi kwa kuzingatia Sheria ya
Mazingira ya mwaka 2004.
Juzi jioni, aliwasili mkoani Tanga kujionea hali ya mazingira na
changamoto za uhifadhi, akitembelea Wilaya ya Pangani na kukagua mradi
wa ujenzi wa Ukuta wa Pangani.
Alimtaka mkandarasi anayejenga ukuta wa mto Pangani Kampuni ya Dezo
Civil Construction Limited kukamilisha ujenzi wa ukuta kwa kipindi cha
miezi 10 kama mkataba unavyoonesha na kuzingatia ubora.
Ujenzi huo wa sehemu ya ufukwe wa kaskazini ambao una urefu wa mita
950 ambazo kati yake mita 550 zipo katika ujenzi wa awali, utagharimu Sh
bilioni 2.4.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdalah alimuomba
Waziri kutuma timu ya wataalamu kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu
kwa fukwe pekee iliyoko katika maeneo ya Tanga DECO ambayo imeathirika
kwa kiasi kikubwa na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na
haipo katika bajeti kwa mwaka huu wa fedha.

0 Comments