Na
Hassan Silayo-MAELEZO
Kuanzia 02 Machi,
2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alianza
ziara ya kikazi ya siku 4 katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara iliyolenga
kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika
mikutano ya hadhara.
Ziara hiyo kwa kiasi
kikubwa imeonesha dira na mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano hasa katika
utekelezaji wa miradi inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali
Imani,kabila na itikadi za vyama vyao vya siasa.
Siku ya kwanza ya
ziara yake Rais Dkt. Magufuli aliweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza
vigae (Tiles) cha Tanzania Goodwill
Ceramic Tiles Ltd. kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani ambacho ni kikubwa
Afrika Mashariki na Kati kilichogharimu Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu
ya kwanza.
Akiongea katika hafla
ya uwekaji wa jiwe la msingi katika kiwanda chenye uwezo
wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku
Rais Magufuli alifurahishwa na teknolojia ya kuyeyusha
mchanga wa kutengenezea vigae inayotumiwa na kiwanda hicho na kuhoji kama kuna
haja ya serikali kuendelea kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi.
Rais Magufuli alisema
kuwa “Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa
kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya
nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa
kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi"
Akiwa njiani kuelekea
Mikoa ya Lindi na Mtwara Rais Magufuli alizungumza na wananchi wa Ikwiriri na
kupokea kero zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha
mradi wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi
Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi wa tatu na kupiga
marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.
Aidha, Rais Dkt.
Magufuli anawataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya
chakula cha kutosha katika kipindi hiki mvua zinaponyesha huku akiweka bayana
kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa ilihali
wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.
Akioneshwa kutoridhishwa
na utekeleaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi alipotembelea ujenzi wa
mradi wa maji wa Ng'apa Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika tangu
tarehe 17 Machi, 2015 Rais Magufuli aliagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria
za mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance
Private Limited ya India Bw. Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo
kampuni hiyo itakapokamilisha mradi huo unaotarajiwa
kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi
wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.
Katika kuthibitisha
amedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda Rais Dkt. Magufuli aliitaka
Wizara ya Nishati na Madini Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inafikisha
gesi katika kiwanda hicho haraka iwezekanavyo lengo likiwa kuondoa vikwazo vya
uhaba wa makaa ya mawe na ukosefu wa gesi ambavyo vimekuwa vikisababisha
uzalishaji wa saruji kusimama mara kwa mara.
Aidha, Dkt. Magufuli
aliitaka Wizara hiyo kuhakikisha wanamega eneo lenye makaa ya mawe katika eneo
la Ngaka lililopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma na kuipatia kampuni ya Dangote
ili iweze kuzalisha yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji
kilichopo Mkoani Mtwara.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa
na Alhaji Aliko Dangote tangu kianze kuuza saruji bei ya bidhaa hiyo sokoni
imeshuka kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja wa kilo 50 hadi kufikia
Shilingi 10,000/- na ununuzi wa magari 580 yatasaidia kusafirisha saruji nchi
nzima kwa gharama nafuu ambayo watanzania wengi wataimudu.
Wakati akikamilisha
Ziara yake Mhe. Dkt. Rais Magufuli alifanya
mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mjini Mtwara ambapo alisema
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inasukuma maendeleo ya Nchi kwa
nguvu kubwa kwa manufaa ya wananchi.
Rais Magufuli alisema
kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutilia mkazo juhudi za uendelezaji
wa bandari ya Mtwara, ujenzi wa barabara, uimarishaji wa miundombinu ya nishati
ya umeme, ujenzi wa viwanda vikubwa na usimamizi mzuri wa shughuli za kilimo
ambavyo vitasaidia kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu.
Aidha, Rais Dkt.
Magufuli alioneshwa kusikitishwa na Mkoa wa Mtwara kufanya vibaya kielimu na
kuwataka kuweka msisitizo katika elimu kwani juhudi za Serikali kuwapelekea
maendeleo hazitakuwa na maana kama wananchi watakuwa hawana elimu.
Ziara hiyo ya Rais
Dkt. Magufuli imeonesha mwelekeo wa Tanzania tunayoitaka hasa katika maeneo ya
usimamizi wa miradi na utekelezaji wake kwa maslahi ya umma.

0 Comments