Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Kutetea
Abiria
(CHAKUA) Hassan Mchanjama (katikati) akiwaonesha waandishi wa habari
(hawapo pichani) baadhi ya vitabu feki vya tiketi
vilivyokamatwa, wakati wa mkutano na waandishi hao leo, Jijini Dar es
Salaam. Kutoka kushoto ni Afisa Miradi wa Taifa wa Chama hicho na Kulia
ni Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Katibu wa Marine Wilson
Sylvester Damo.
Picha Na. Husna Saidi
...
Chama cha Kutetea Abiria
Tanzania (CHAKUA) kimeishauri Serikali kuanzisha mfumo wa kukata tiketi kwa
njia ya mtandao ili kudhibiti tiketi feki zinazotolewa na baadhi ya mabasi
yaendayo mikoani katika stendi kuu ya
mabasi ya Ubungo, Jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti
Taifa wa CHAKUA, Hassan Mchanjama alipokuwa akiongea na waandishi wa habari
kuhusu utoaji wa tiketi feki kwa mabasi yaendayo mikoani, leo Jijini Dar es
Salaam
Mchanjama alisema kuwa, Aprili
21 mwaka huu chama hicho kiliiandikia barua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yenye
kumbukumbu namba CHAKUA/KMN/04/2017 kuiomba Serikali kuanzishA mfumo mpya wa
ukataji tiketi kwa njia ya mtandao ili kuepukana na ubababishaji, utapeli na
wizi wa kila siku unaofanywa na baadhi ya Mawakala, Makarani na wapiga debe
katika stendi zote nchini Tanzania.
“Kumekuwa na wimbi kubwa la
tiketi feki ambazo hutolewa na mawakala wa mabasi katika stendi ya mabasi ya Ubungo
na Mbeya, hiyo ni kutokana na kukamatwa kwa baadhi ya vitabu vya tiketi ambavyo
vimefojiwa TIN namba bila kibali kutoka TRA”, alisema Mchanjama.
Aliongeza kwa kusema, mfumo huo
wa ukataji wa tiketi kwa njia ya mtandao utasaidia kuokoa muda, kuondoa kero za
abiria kuibiwa, kuwabana Mawakala na Makarani ambao wamakuwa wakitoroka na
mauzo ya tiketi, wamiliki kupata pesa zao kwa uhakika, kujua idadi kamili ya
abiria waliokuwepo ndani ya basi husika, kujua idadi ya watu waliopoteza maisha
na majeruhi pindi ajali zinapotokea pamoja na kusaidia Serikali kukusanya kodi
kwa urahisi na uhakika.
Aidha, CHAKUA imefanya utafiti
kwa muda mrefu na imegundua njia pekee ya kuondoa matatizo hayo ni kuhama katika
mfumo unaotumika sasa na kuingia kwenye mfumo wa mtandao (ki-electronic) ambao
una mafanikio na ufanisi mkubwa hususani unaotumika katika mabasi ya mwendokasi
UDART (BRT).
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Kanda ya Mashariki na Katibu wa Marine, Wilson Sylvester Damo aliwataka abiria
kuwa na mazoea ya kukata tiketi kwenye sehemu husika zinazojulikana kisheria
ili kuepukana na usumbufu unaojitokeza.
Nae, Katibu Idara ya Reli
Maulid Masalu aliwataka waandishi wa habari kushirikiana kwa ukaribu na CHAKUA
kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na faida ya utumiaji wa mfumo wa kukata tiketi
kwa njia ya mtandao kwani ni salama zaidi.

0 Comments