Na Husna Saidi-
MAELEZO
Takribani shilingi milioni 271 zinadaiwa
kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma Mjini, Mkoani Mara ikiwa ni kodi ya Pango la
Ardhi.
Hayo yamebainishwa na
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipofanya
ukaguzi wa mfumo wa kodi ya ardhi hivi karibuni Mkoani humo.
Waziri Lukuvi alisema kuwa
amekagua mfumo wa kodi wa manispaa ya Musoma mjini ili kuhakikisha wamiliki
wote wa ardhi nchini wanalipa kodi kwa hiari kabla ya hatua za kisheria
hazijafuata dhidi yao.
“Nimeagiza kesi za madai ya
kodi zitolewe hukumu ndani ya siku moja tu ili wadaiwa waweze kuchukuliwa hatua
ya kuuzwa kwa mali zao haraka”, alisema Lukuvi.
Aidha Waziri Lukuvi alimtaka Afisa
Ardhi wa Manispaa ya Musoma Bw.Joseph Kamonga kuwasilisha majina ya wadaiwa hao
katika Mahakama ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na
kupiga mnada majengo na mali zao kama wakikaidi kulipa kodi hiyo.
Kwa upande mwingine Lukuvi
alifanya uzinduzi wa mpango kabambe (Master Plan) wa Manispaa ya Musoma na kuwapongeza
viongozi na watendaji wa Manispaa hiyo kwa kuwa Manispaa ya kwanza nchini
kuweza kuzindua mpango huo kutumia kampuni za ndani katika utekelezaji wa
mpango huo.
Kufuatia hatua hiyo Waziri
Lukuvi amezitaka Manispaa nyingine kutumia kampuni za ndani ya nchi ambazo
zimesajiliwa na Wizara ya Ardhi katika
kutekeleza mipango mbalimbali ya ulipaji kodi za ardhi.
Pia Waziri Lukuvi aliiagiza Manispaa
ya Musoma kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa mpango kabambe kwa kutumia
wataalam wao (wa serikali) au Makampuni ya ndani na kutoa nakala za kutosha ili
mpango huo uwafikie wadau wote na kutaka mpango huo utafsiriwe kwa Kiswahili
ili Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa waweze kuwafikishia wananchi kwa
urahisi.

0 Comments