Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga akizungumza na wananchi, kata ya Njianne wilayani hapo.
Katibu wa siasa na uenezi mkoani Pwani, dk. Zainab Gama akiongea jambo huko kata ya Njianne wilaya ya Mkuranga.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mkuranga Abihudi Shilla akizungumza
Wakazi wa kata ya Njianne na wanaCCM wakisikiliza jambo wakati mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga akizungumza.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
............
Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga
MKUU wa wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Filberto Sanga amewataka wazazi ambao watoto wao wamefaulu kuingia kidato cha kwanza kuwapeleka shule mara moja, na atakaebainika kukaa na mtoto nyumbani atakiona.
Aidha amewataka wazazi wenye watoto
waliofikia umri wa kuanza darasa la kwanza kwenda kuwaandikisha bila kufanya
ajizi.
Amesema kuanzia sasa
ataambatana na timu yake, kupita kuhakiki kijiji hadi kijiji na endapo atakutwa
mtoto hajapelekwa shule mzazi wake atafikishwa mahakamani.
Sanga alisema msimamo
huo,wakati akizungumza katika kata ya Msonga, Magawa, Njianne, Kitomondo na
Mwarusembe wilayani hapo kwenye mikutano ya ndani iliyoandaliwa na Chama Cha
Mapinduzi Mkoa wa Pwani.
Alieleza licha ya
serikali kuagiza elimu kutolewa bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha
nne lakini wapo wazazi mpaka sasa wanaoshindwa kuwapeleka shule watoto
wao kwa sababu zisizoeleweka.
Sanga alisema atalivalia
njuga suala hilo hadi hapo atakapohakikisha watoto hao wameripoti mashuleni.
Alifafanua kwamba sekta
ya elimu haina utani hata kidogo na ni haki ya mtoto Sanga alibainisha kwamba,
watoto bila kuwa na elimu wilaya hata mkoa na taifa haitojikomboa.
"Asilimia 80 ndio
walioripoti mashuleni wengine wapo majumbani ,hivyo wazazi wawe na mwamko wa
elimu ili kuwakomboa watoto wao”
“Serikali inachangia vitu
vyote vya msingi ,sioni sababu ya mzazi kukaa na bila elimu, atakaekaidi agizo
hili afikishwe mahakamani”alisisitiza Sanga.
Kwa upande wake,katibu wa
siasa na uenezi CCM mkoani Pwani, Zainab Gama, aliwataka wazazi kuwalinda na
kuwalea watoto kwa umoja kwani mtoto wa mwenzio ni wako.
Alisema vijana wengi
wanaharibika kutokana na kuiga maadili ya nchi za nje na kushawishiana.
Gama aliiomba jamii
kukemea watoto na vijana ambao wanakiuka mila, desturi na maadili ya nchi bila
kuwaonea aibu.
Nae katibu wa CCM wilaya
ya Mkuranga, Abihudi Shilla alisema anaunga mkono suala la watoto kufikishwa
shule kwa wakati kwa kuwa anatambua umuhimu wa elimu.
Shilla anasema, endapo
watu wanachangia harusi na sherehe kuna kila sababu ya kuipa kipao mbele
elimu ili kuwajengea watoto msingi bora katika maisha yao ya baadae.




0 Comments