Mwanachama na kijana tajiri barani Afrika kwa sasa Mohammed
Dewji anayetaka kununua hisa Simba, amesikitishwa na uongozi wa klabu
hiyo kwa kuingia mkataba wa udhamini na kampuni ya SportPesa bila
kumshirikisha.
Habari ambazo
hazijathibitishwa na upande wowote, zinasema Mo Dewji, Mbunge wa zamani
wa Singida Mjini ameuandikia barua uongozi wa klabu hiyo chini ya Rais
wake, Evans Aveva kudai alipwe fedha zake, Sh Bilioni 1.4 alizokuwa
anaikopesha Simba kwa kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la Ufundi,
Sh Milioni 80 kila mwezi.
Imedaiwa Mo Dewji alikuwa anatoa fedha hizo kwa makubaliano
zitalipwa wakati mpango wake wa kununua hisa za klabu utakapokamilika.
Mo alikubaliana na uongozi wa Simba kununua asilimia 51 ya hisa kwa Sh.
Bilioni 20 mara baada ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba
utakapokamilika.
Lakini zoezi hilo linaelekea
kuingia doa baada ya Mo Dewji kuandika katika ukurasa wake wa Twitter
akilalamikia uongozi wa klabu kuingia mkataba na SportPesa bila
kumshirikisha.
Na upande mwingine, uongozi wa Simba na umemeguka baada ya
Mjumbe wa kuteuliwa wa Kamati ya Utendaji wa usajiri, Zacharia Hans
Poppe ameandika barua ya kujiuzulu, naye pia akilalamikia
kutoshirikishwa katika mkataba wa SportPesa.
Hans Poppe aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati za Usajili na
mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Bunju Complex, amethabitisha kujiuzulu
kwake, lakini hakutaka kuzama ndani zaidi juu ya sakata hilo.
Ijumaa SportPesa Tanzania ilitangza rasmi udhamini wake wa
miaka mitano kwa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, wenye thamani ya Sh.
Bilioni 4.96.
Mkurugezi wa Utawala wa SportPesa, Tarimba Abbas alisema kwamba
wameingia mkataba huko kwa dhumuni la kuendeleza soka nchini na
kuisaidia klabu ya Simba kufikia malengo yake.
Akifafanua, Tarimba ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa mahasimu
wa Simba, Yanga alisema kwamba, katika mkataba wao kwa mwaka wa kwanza
wadhamini hao watatoa Sh. Milioni 888 na miaka itakayofuata wataongeza
asilimia 5 na miaka miwili ya mwisho watatoa Sh. Bilioni 1 na kwamba
fedha hizo zitatolewa kwa awamu nne kwa mwaka.
Tarimba alisema kwamba Simba watapaswa kuyathibitisha matumizi ya fedha hizo kwamba yalifanyika kwa maendeleo ya soka.
Alisema licha ya mkataba huo, pia kutakuwa na motisha klabu
hiyo ikishinda mataji, mfano kwa ubingwa wa Ligi Kuu watapewa zawadi ya
Sh. Milioni 100.
“Pia ikishinda michuano kama (Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati) Kombe la Kagame pia watapewa zawadi na wakifanya vizuri katika
Ligi ya Mabingwa Afrika watapata zawadi ya Milioni. 250,”alisema
Tarimba.


0 Comments