Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Profesa Samwel Manyele (wa pili
kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini
Dar es Salaam kuhusu kampuni ya TECHNO NET SCIENTIFIC kukutwa na
kemikali bashirifu bila kuwa na usajili wala kibali cha kufanya shughuli
za kuuza na kusambaza kemikali. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya
Huduma za Ubora wa Bidhaa, Bw. Daniel Ndiyo, Mkurugenzi wa Idara ya
Maendeleo ya Biashara Bw. George Kasinga na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi
Idara ya Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba. Bi. Hadija Mwema
Baadhi ya waandishi wa habari
waliohudhuria mkutano wa Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Profesa Samwel
Manyele (hayupo pichani) leo Jijini Dar es Salaam uliohusu kampuni ya
TECHNO NET SCIENTIFIC kukutwa na kemikali bashirifu bila kuwa na usajili
wala kibali cha kufanya shughuli za kuuza na kusambaza kemikali.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Kampuni ya Techno Net
Scientific inayojishughulisha na uingizaji pamoja na uuzaji wa kemikali
imekutwa na kemikali zilizoingizwa nchini kwa njia za udanganyifu kwa
kutumia vibali vya bandia.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar
es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Prof. Samwel Manyele
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampuni hiyo kukutwa
na kemikali bashirifu bila kuwa na usajili wala kibali cha kufanya
shughuli za kuuza na kusambaza bidhaa hiyo.
Prof. Manyele amesema kampuni hiyo
ilikuwa na usajili wa miaka miwili kuanzia April 30 mwaka 2014 hadi
Aprili 30, 2016 ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali kampuni hiyo
ilipaswa kusitisha shughuli zake hadi pale cheti cha usajili
kitakapopatikana.
“Ingawa shughuli zake zilisitishwa
lakini kampuni hiyo iliendelea kufanya kazi bila kuwa na cheti cha
usajili hivyo ofisi yangu iliungana na Mamlaka ya Kudhibiti dawa za
kulevya na Mamlaka ya Chakula na Dawa kufanya ukaguzi wa pamoja ambapo
kwa sasa tumewaachia vyombo vya dola kufanya uchunguzi wao” amesema Prof
Manyele.
Amefafanua kuwa Sheria ya Kemikali
za Viwandani na Majumbani Sura ya 182 na kanuni zake inatoa masharti
kuwa kila mtu anayetaka kujihusisha na shughuli za kemikali kwa namna
yoyote ni sharti awe amesajiliwa na kufanyiwa ukaguzi.
Aidha, ametoa rai kwa
wafanyabiashara wote wa kemikali na umma kwa ujumla kuwa Serikali
haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa makampuni na wafanyabiashara
wasiokuwa waaminifu na wanaovunja matakwa ya Sheria katika uingizaji,
usafirishaji, uhifadhi na utumiaji wa kemikali ikiwemo kemikali
bashirifu nchini.
Prof. Manyele amewaomba wananchi
kutoa taarifa na kuwafichua wafanyabiashara wa kemikali wanaokiuka
matakwa ya Sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria
ambazo zitapelekea wengine kuwa na matumizi salama ya kemikali na kuzuia
madhara kwa watu na mazingira.


0 Comments