Aliyekuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tatu, Frederick
Sumaye amejitoa katika Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB kwa madai
kuwa familia yake inafuatwafuatwa hivyo kuhofia kuwa anaweza kuathiri
benki hiyo.
Baada ya kujitoa kama mmoja wa viongozi wa benki hiyo kubwa nchini,
Sumaye amesema kuwa ataendelea kuwa mwanahisa wa benki hiyo ya
biashara.
“Sitaki msimamo wangu wa kisiasa uhusishwe na benki yetu” alisema
Sumaye ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na Mwenyekiti wa
CHADEMA Kanda ya Pwani.
Sumaye alisema kuwa huenda majukumu yake ya kisiasa yakambana na
akashindwa kuhudhuria baadhi ya vikao muhimu vya benki hiyo ambavyo ni
muhimu kwa ufanisi na ustawi wa benki.
Akiwa nje ya mkutano huo Sumaye alisema kuwa, familia yake imekuwa
ikifuatwafuatwa na serikali na kwamba tayari mtoto wake amepokwa shamba.
Serikali pia alimnyang’anya Sumaye shamba lake lililokuwa
Mabwepande kwa madai hakuliendeleza, huku yeye akisema uamuzi wa yeye
kupokwa shamba ulikuwa ni wa kisiasa. Sumaye alieleza kwamba hakuweza
kulima shamba hilo kutokana na serikali kupiga kilimo jijini Dar es
Salaam.
Sumaye amesema uamuzi wake aliuchukua ili CRDB iweze kuendeshwa na
watu walioko huru mbele ya jamii kuepusha hisa za wafanyabishara wengine
kuathiriwa.
Sumaye anamiliki zaidi ya hisa milioni 7.4 za benki hiyo.

0 Comments