Na Daudi
Manongi,MAELEZO,DODOMA.
Serikali kupitia
Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo imesema kuwa inakamilisha mapitio
ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 ili kuhakikisha inaendana na
mahitaji ya sasa katika maendeleo ya michezo nchini.
Hayo
yamebainishwa na Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo
Mhe.Anastazia Wambura wakati akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini
Mhe.Cosato Chumi aliyetaka kujua mipango ya Serikali katika kufufua mchezo wa
Riadha Bungeni Mjini Dodoma leo.
“Serikali kwa
kushirikiana na wadau inatekeleza programu mbalimbali za kuendeleza mchezo wa riadha nchini ikiwemo Kilimanjaro
Marathon,Bagamoyo Marathon,Heart Marathon na Tulia Marathon ambayo hushirikisha
wanariadha kutoka nje”,Aliongeza Mhe.Wambura.
Aidha pamoja
na hayo Mhe.Wambura amesema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya
Elimu,Sayansi na Teknolojia pamoja na
Ofisi ya Rais TAMISEMI imeendesha mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA ambayo pamoja na mambo mengine yanalenga
kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wetu katika mchezo wa riadha.
Akizungumzia suala
la miongozo ya Kiserikali amesema kuwa Wizara yake inakamilisha taratibu za
kuandaa miongozo ya kiserikali ili kuwezesha wadau wote kuendesha shughuli
zao katika mazingira ya weledi na stadi bora za michezo.
Hata hivyo
Naibu Waziri uyo amesema kuwa nchi yetu imeanza kufanya vizuri katika
mashindano ya Riadha kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma kupitia kwa
wanariadha wake kama Francis Naal,Samson Ramadhani,Gidamis Shahanga,Juma Ikangaa,Suleiman
Nyambui na Filbert bayi na hivyo kuitangaza nchi yetu.
“Nchi yetu kwa
sasa imeanza kupata mafanikio katika riadha kupitia wanariadha wetu kama
Alphonce Simbu aliyeshinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya standard Chartered
Mumbai Marathon,Cecilia Ginoka Panga aliyeshinda Beijing International Half
Marathon na Giniki Gisamoda aliyeshinda Shanghai International Half
Marathon,wote hawa wanaitangaza nchi yetu vizuri na kuifanya ifahamike na hivyo
kuvutia watalii ”Alisisitiza Mhe.Wambura.

0 Comments