Mwenyekiti Mteule wa Kamati ya Kuchunguza Mkataba wa Ubia baina ya TBC na Kampuni ya Startimes, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi
Na.
Mwandishi Wetu
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ameunda Kamati ya wajumbe kumi
itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi,
kuchunguza ufanisi katika mkataba baina ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC)
na Kampuni ya Star Times.
Taarifa iliyotolewa leo
na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inaeleza
kuwa mbali na Dkt. Abbasi, wajumbe wengine wanaunda Kamati hiyo kutoka upande
wa Tanzania ni Bw. Kyando Evod kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Bw. Frederick Ntobi na Injinia James Kisaka wote kutoka Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Bw. Mbwilo Kitujime kutoka TBC.
Aidha, taarifa hiyo
imeeleza kuwa majina ya wajumbe wengine watano walioteuliwa kutoka upande wa
China yatawasilishwa ili kukamilisha idadi ya wajumbe kumi wa Kamati hiyo.
“Kamati imepewa
hadidu za rejea takribani nane na inatakiwa kufanya kazi kwa muda wa siku saba
kukamilisha kazi hiyo”, inaeleza taarifa hiyo.
Kamati hiyo imeundwa
kufuatia kutopatikana kwa faida kwa kipindi cha miaka saba sasa katika mkataba
baina ya TBC na Kampuni ya Star Times.
Kabla ya kuunda
Kamati hiyo, jana Waziri Mwakyembe alikutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Star
Times kutoka China, Xinxin Pang kujadiliana kwa kina juu ya mkataba huo ambapo
katika majadiliano hayo walikuwepo wafanyakazi wa Wizara hiyo akiwemo Katibu
Mkuu, Profesa Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO)
Dkt. Abbasi.
Sakata la mkataba
baina ya TBC na Star Times lilichukua sura mpya baada ya Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kutembelea ofisi za TBC mwezi Mei mwaka huu na kuonesha kukerwa na
kutopatikana kwa faida katika mkataba huo kwa kipindi cha miaka saba na kuagiza
kuchukuliwa kwa hatua stahiki.

0 Comments