WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa
maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya ya Rungwe
mkoani Mbeya ilitengewa sh. bilioni 2.72 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji.
Amesema mkakati
huo unatekelezwa kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama
ndoo, wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama
katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Waziri Mkuu
aliyasema hayo jana (Jumapili, Julai 30, 2017) alipozungumza kwa nyakati
tofauti na wananchi wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo katika mikutano ya
hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale katika wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.
Alisema mkoa wa
Mbeya umetengewa sh. bilioni 10.383 kwa
ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji, ambapo kati yake sh. bilioni 2.72
zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye wilaya ya
Rungwe.
Waziri Mkuu
alitaja mradi mwingine unaotekelezwa wilayani Rungwe ni pamoja na mradi wa maji
wa Masoko wenye thamani ya sh. bilioni 5.3, utakaohudumia jumla ya vijiji 15.
“Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayojengwa chini ya Programu ya Maendeleo ya
Sekta ya Maji kwa fedha za ndani.”
Alisema mradi huo utakapokamilika
utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika
vijiji vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi,
Nsyasa, Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga.
Pia Waziri Mkuu
alisema wananchi lazima
wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja
na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Kufuatia hali
hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji kuwachukua hatua watu wote watakaokutwa
wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji
wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.
“Hatuwezi
kuruhusu Taifa likaangamia kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu mazingira kwa
kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji. Ni marufuku kufanya shughuli za kibinadamu
ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji, atakayekutwa atachukuliwa hatua
za kisheria.”
Awali
Mbunge wa Jimbo la Busokelo Mheshimiwa Fredy Mwakibete na mbunge wa Rungwe
Mheshimiwa Saul Amon walimueleza Waziri Mkuu kwamba upatikanaji wa huduma ya
maji na salama ni miongoni mwa changamoto zinazoyakabili majimbo yao.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
JULAI 31, 2017

0 Comments