Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Young Human Rights Advocates (TYHRA) Samwel Shami akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari kuhusu wachimbaji wadogo wa dhahabu kumpongeza Rais Magufuli leo Jijini Dar es Salaam.
Na. Neema Mathias- MAELEZO
......................
Wachimbaji
wadogo wa dhahabu kutoka wilaya ya Kahama wanatarajia kutembea kwa miguu kutoka
Kahama mpaka Dar es salaam kwa ajili ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za kuijenga Tanzania mpya.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Young Human
Rights Advocates (TYHRA) Samwel Shami kwa niaba ya wachimbaji hao, alipokuwa akizungumza
na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam.
“Tumeamua
kwa hiyari yetu kutembea kwa miguu na baiskeli kutoka Kahama mpaka Dar es
Salaam kumpongeza Rais wetu mpendwa na tunaomba Watanzania wenzetu wanaoipenda
nchi yetu watuunge mkono”, alisema Bw. Shami.
Bw.
Shami amesema kuwa wachimbaji hao wamefurahishwa na juhudi za serikali ya awamu
ya tano pamoja na moyo wa utu wa Mhe. Raisi katika kuhakikisha rasilimali za
Tanzania zinawanufaisha Watanzania wote.
“Kuna
wakati tulijiona kama yatima kwenye nchi yetu, na tulianza kuamini kuwa dhahabu
yetu imegeuka laana badala ya baraka alizotupatia mwenyezi Mungu bure, lakini
sasa tunaiona nuru kubwa kupita Raisi wetu”, amesisitiza Bw. Shami.
Aliendelea
kusema kuwa mwaka 2008, Shirika la TYHRA kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo,
wadau wa maendeleo na wafanyakazi wa mgodi wa Bulyanhulu walianzisha harakati zilizojulikana kama ‘Native
Solidarity Movement’ kwa lengo la kudai haki zao za msingi katika migodi lakini
hazikuzaa matunda.
Hata hivyo Bw. Shami ameyaomba mashirika
mengine yasiyo ya kiserikali na yeyote anayeitazama Serikali kwa jicho la
maendeleo na mwenye mapenzi mema na nchi yake wajaribu kutumia nguvu kubwa
kuipongeza, kuishauri na kuitia moyo serikali kama wanavyotumia nguvu kubwa
kukosoa na kulaani mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali.
Bw. Shami alifananisha matatizo na changamoto
za Watanzania sawa na kupewa tembo mkubwa kumla, jambo ambalo linahitaji hatua
kwa hatua, kipande kwa kipande, hivyo aliwataka Watanzania wampe Rais muda wa
kutatua changamoto zao kwani juhudi zake
zimeonekana toka alipoingia madarakani.
Shirika
la Young Human Right Advocates linajihusisha na utetezi wa haki za binadamu na
wadau wa maendeleo. Shirika hilo linashirikiana na wachimbaji wadogo wa wilaya
ya Kahama kuchangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa na pia kukemea na
kuelimisha jamii.

0 Comments