Na Daudi Manongi,MAELEZO,DODOMA.
Waziri Mkuu
Mhe.Kassim Majaliwa ameelekeza Baraza la
Michezo Tanzania(BMT) livunjwe na shughuli zake kufanywa na Sekretarieti hadi
hapo Baraza jipya litakapoundwa tena.
Waziri Mkuu
ametoa maagizo hayo leo Bungeni Mjini Dodoma wakati akisoma hotuba ya kuhairisha mkutano wa saba wa Bunge la kumi na
moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Serikali ya
awamu ya tano haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo
usiojali maslahi ya Taifa,Serikali
imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya michezo nchini ili kila mwenye
dhamana awajibike ipasavyo”,Aliongeza Mhe.Majaliwa.
Aidha katika
hotuba yake amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dk John Pombe
Magufuli kwa kuunga mkono jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya
kujenga Uwanja mkubwa wa Michezo hapa mjini Dodoma kwa kushawishi mataifa rafiki kama vile
Moroco ambao wanajenga uwanja huo.
Pia amesema
kuwa Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa Afya,umoja wa kitaifa na kama
fursa ya ajira kwa vijana wetu ambapo ivi karibuni mkoani Mwanza yamehitimishwa mashindano ya
UMISSETA na UMITASHUMTA yaliyoibua
vipaji na hamasa kubwa iliyo miongoni
mwa vijana nchini.
“Tutaendelea
kuratibu michezo shuleni,ikiwa ni pamoja
na kusimamia ufundishaji wa michezo kama somo,maelekezo yetu ni kwamba kila
mkoa uwe na shule angalau mbili zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa
stahiki za kufundisha michezo,Ameeleza Mhe.Majaliwa.
Waziri Mkuu
Majaliwa pia ameipongeza kwa dhati timu ya Serengeti Boys kwa kutoa upinzani
mkubwa kwenye mashindano ya shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika na
kuweka msisitizo kwa Chama cha Mpira nchini(TFF) kuendelea kuwatunza vijana
hao.
“Msisitizo wangu
kwa TFF ni kuendelea kuwatunza vijana hao na kusimamia vilabu vya michezo
nchini, kuwekeza kwenye soka la vijana ili kujenga timu imara kwa miaka
michache ijayo”,Aliongeza Mhe.Majaliwa.
0 Comments