Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga
(aliyesimama) akifungua Warsha ya Siku Mbili ya Wadau wa Vyama vya Ushirika
inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Benki Kuu Tawi la Mtwara, Bw. Lucas Mwimo
(kushoto) na Kaimu Katibu Tawala Msaidizi – Uchumi na Uzalishaji, Bw. Amani
Rusake (kulia).
Mwakilishi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini, Bw.
Nerei Kyara akizungumza na Wadau wa Vyama vya Ushirika wakati wa Warsha ya Siku
Mbili ya Wadau inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Mtwara. Wengine pichani ni Kaimu Katibu Tawala Msaidizi – Uchumi na
Uzalishaji, Bw. Amani Rusake (kushoto) na Mkuu wa Kilimo na Fedha Vijijini wa Mfuko
wa Kukuza Sekta ya Fedha, Bw. Mwombeki Baregu.
Wadau wa Vyama vya Ushirika wakifuatilia mijadala
mbalimbali wakati wa Warsha ya Siku Mbili ya Wadau inayoendelea katika Ukumbi
wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Wadau wa Vyama vya Ushirika wakiwa katika picha ya
pamoja mara baada ya ufunguzi wa Warsha ya Siku Mbili ya Wadau hao inayoendelea
katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
..................
Na Mwandishi wetu, Mtwara
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewaasa
wakulima wa korosho nchini kuongeza uzalishaji wa korosho ili kuchangamkia
fursa za masoko ya zao hilo linalohitajika zaidi katika masoko ya Marekani,
Vietnam na India.
Wito huo umetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa TADB, Bw. Francis Assenga wakati akifungua Warsha ya Siku Mbili ya Wadau wa
Vyama vya Ushirika inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Mtwara.
Bw. Assenga alisema kuwa mahitaji ya korosho ni
makubwa sana katika soko la dunia hivyo wakulima wa zao hilo hawana budi
kujizatiti ili kuhakikisha wanazalisha kiasi kikubwa cha korosho ili kufikia au
kuzidi malengo ya mavuno kwa msimu ujao ambayo yanakadiriwa kufikia kati ya
tani laki tatu (3) hadi laki nne (4) ukilinganisha na takribani tani laki mbili
na nusu kwa msimu uliopita.
Bw.
Assenga alisema kuwa korosho ni zao la kimkakati ambalo likiwekezwa kwa usahihi
linaweza kunyanyua uchumi na kipato kwa wakulima wa mikoa ya kusini na pwani
ambao niyo ni wazalishaji wakuu wa zao hilo.
“Nawaasa
mujitahidi kulima kisasa ili kuweza kufikia au kuvuka malengo ya mavuno ya
msimu huu hali itakayowaongezea kipato hivyo kufikia malengo ya serikali ya
kuwanyanyua wakulima nchini,” alisema.
Kaimu
Mkurugenzi huyo wa TADB aliongeza kuwa Benki yake imejipanga kusaidia mfumo wa
Stakabadhi ya maghala ili kuhakikisha kuwa malengo ya mavuno ya korosho kwa
msimu huu yanafikiwa.
“TADB
iko tayari kuratibu mfumo wa malipo ya fedha zitokanazo na mauzo ya korosho kwa
njia ya TEHAMA, pia kwa kushiriakiana na soko la mazao (TMX), kusimamia ununuzi
wa mazao kwa njia ya mtandao (electronic auction),” aliongeza
Aliongeza
kuwa Benki ipo tayari kusimamia uuzaji wa mazao kwa mifumo ya salama ya
kimataifa ya malipo kama vile dhamana ya malipo.
Naye
Mkurugenzi wa Biashara wa Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha alisema kuwa
Benki ya Kilimo ipo tayari kutoa mikopo kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu
ya umwagiliaji na maghala na uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya korosho na mihogo.
Aliongeza
kuwa TADB pia ipo tayari kuviwezesha viwanda vya kubangua mazao ya
korosho, na kusindika ufuta, mihogo pamoja na uanzishaji wa mashamba mapya na
ya kisasa ya korosho na ufuta.
“Tupo
tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kuwanyanyua wakulima kama ilivyolengwa na
Serikali kupitia mikopo ya pembejeo kuongeza tija kwenye uzalishaji, miundo
mbinu ya umwagiliaji na ununuzi wa zana za kilimo (kama matrekta, pump),”
alisema.
Bw.
Chacha aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mazao ya kilimo, Benki
ya Kilimo ipo tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kujenga maghala mapya au
kuboresha yaliyopo pamoja na kununua mizani ya kisasa na ununuzi wa magari ya
usafirishaji mazao.
0 Comments