Mratibu
na Mtendaji Mkuu wa Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA) Bw. Monday Likwepa
akielezea changamoto zinazowakabili abiria mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo
pichani), katikati ni Mwenyejkiti wa Chama hicho Bw. Hassan Mchanjama, kulia ni
Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Katibu wa Marine Bw. Wilson Sylvester Damo.
Mwenyekiti
wa Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA) Bw. Hassan Mchanjama akitoa ufafanuzi juu
ya ukataji tiketi kwa njia ya kieletroniki kwa wasafiri alipokuwa akizungumza
na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), wa kwanza kutoka Kushoto ni Afisa
Miradi Taifa wa Chama hicho Bw. Elias Kalinga, katikati ni Mratibu Mtendaji
Mkuu wa Chama hicho Bw. Monday Likwepa.
Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
................................
Na, Neema Mathias & Thobias Robert -MAELEZO
Chama cha Kutetea Abiria
(CHAKUA), kimeanzisha mikakati mbalimbali itakayotumika kukabiliana na
changamoto zinazowakumba wasafiri wa majini na nchi kavu hapa nchini.
Hayo yamesemwa Leo Jijini Dar es Salaam na
Mratibu Mtendaji wa CHAKUA Bw. Monday Likwepa alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazowakabili abiria na namna ya
kuzikabili, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
kila abiria anapata haki yake hasa pale anapopata tatizo akiwa safarini kwa
kutumia chombo cha moto au anapokuwa akitembea kwa miguu.
Likwepa alisema kuwa changamoto hizo ni pamoja
na abira kulanguliwa wanapokata tiketi kwaajili ya safari, kuibiwa fedha,
kupoteza mizigo, kulala mahali pasipostahili, kukosa huduma za matibabu na
fidia wanapopata ajali pamoja na njaa ya kutwa nzima kwa kukosa huduma ya
chakula na vinywaji ndani ya vyombo husika vya usafiri.
“kutokana na changamoto hizo
CHAKUA tumekuja na mikakati ya kuhakikisha kuwa abiria anayepata ajali na
kusababisha ulemavu wa kudumu au kupoteza maisha anapata haki na fidia stahiki,
kusimamia kesi zote mahakamani pamoja na kuelimisha abiria kujua haki na wajibu
wa msafiri na msafirishaji mjini na vijijini kwani abiria wengi wameonekana
kutokuwa na elimu ya kutosha jambo ambalo linapelekea kukosa haki zao za
msingi,” alifafanua Likwepa.
Licha ya CHAKUA kuonyesha
jitihada mbalimbali za kumtetea abiria, wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la
ukosefu wa rasilimali fedha kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia fedha zao
binafsi kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili abiria jambo ambalo limekuwa
likiwaelemea kwani changamoto za abiria huongezeka siku hadi siku.
“Kwa mujibu wa katiba ya CHAKUA
vyanzo vya mapato yake ni ada za wanachama, wadau, na wahisani. Michango hii
imekua haitoshelezi kutekeleza majukumu yao ya kila siku, hivyo ili kutekeleza
majukumu yake kikamilifu CHAKUA inamwomba kila Mwanachama alipe ada zake na
kila abiria anaposafiri atalazimika kulipa sh 200 ili kukiwezesha chama hicho
kutekeleza majukumu yake ipasavyo,”alieleza Likwepa.
Likwepa alifafanua kuwa kupitia
kupitia sh 200 ambayo itakua inalipwa na wasafiri wa mabasi na treni za mikoani
itawawezesha kujenga ofisi zao katika vituo vyote vya usafiri nchini, halikadhalika
fedha hizo zitatumika kuwasaidia wasafiri pale wanapopata matatizo mbalimbali, mkakati
huu utaanza rasmi pale mamlaka zinazohusika na usafiri zitakaporidhia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
CHAKUA Bw. Hassan Mchanjama ameitaka Serikali kuwalazimisha wenye mabasi ya abiria kutumia
mfumo wa kielektroniki katika ukataji wa tiketi kwa wasafiri ili kudhibiti tatizo la ukwepaji kodi ambao
umekua ukifanywa na baadhi ya wamiliki wa mabasi kupitia Chama cha Wamiliki wa
Mabasi (TABOA).
“TABOA wamekuwa wakipinga mfumo
wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroniki ili kuendelea kuwalangua abiria na
kukwepa kutoa mapato sahihi kwa serikali,” alieleza Mchanjama na kusisitiza, “serikali
haina budi kukifuta chama hicho kwani wengi wanaounda kikundi hicho sio wamiliki
wa mabasi badala yake TABOA wameweka madalali ambao ndio wanaohudhuria vikao
vya serikali.”
Aidha Mchanjama ameiomba serikali
iwachunguze TABOA kwani wamekua wakitumia vyombo vya habari kupotosha na kwenda
hadi kwa viongozi wa Serikali Dodoma ili kuchelewesha zoezi la abiria kukatiwa
tiketi kwa mfumo wa kielektoniki, hivyo serikali haina budi kukifuta chama
hicho kwani wanaongoza kwa propaganda, hujuma, fitina hata kudiriki kutoa
rushwa ili kuchelewesha kuanzishwa kwa mfumo huo.
CHAKUA kilianzishwa kwa malengo ya kutoa
huduma mbalimbali kwa wasafiri wanaopata adha katika safari zao na kimesajiliwa
kwa mujibu wa Sheria ya usafiri wa nchi kavu na majini, Chama hiki kipo chini
ya SUMATRA kwa ushirikiano mkubwa wa Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za
kiserikali na kijamii.

0 Comments