Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe akichomoa gazeti jipya la Michezoa la Mwanaspoti ambalo lina
muonekano mpya wa kisasa zaidi mara baada ya kulizindua Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe pamoja na baadhi ya Viongozi waandamizi wa Kampuni ya
Uchapishaji Magazeti ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) wakishangilia mara
baada ya uzinduzi wa Muonekano Mpya wa Gazeti la Michezo la Mwanaspoti Jijini
Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe akibofya kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa Muonekano Mpya
wa Gazeti la Michezo la Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia tukio
hilo ni baadhi ya Viongozi waandamizi wa Kampuni ya Uchapishaji Magazeti ya
Mwananchi Communications Ltd (MCL).
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uchapishaji
Magazeti ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bw. Francis Nanai (kulia) wakiwaonyesha
Waandishi wa habari muonekano mpya wa gazeti la michezo la Mwanaspoti mara baada
ya uzinduzi Jijini Dar es Salaam.
.......................
Na
Benedict Liwenga-WHUSM.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameipongeza Kampuni
ya Uchapishaji Magazeti ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa jitihada
kubwa wanazozifanya katika kusimamia maadili kwa kuhabarisha na kuielimisha
jamii ya Kitanzania.
Pongezi hizo amezitoa
jana wakati wa Uzinduzi wa Muonekano Mpya wa gazeti pendwa la michezo la Mwanaspoti
linalochapishwa na Kampuni hiyo.
Dkt. Mwakyembe
amesema kuwa, mara kwa mara MCL imekuwa ikiisaidia jamii kwa kujihusisha katika
masuala mbalimbali ya kijamii kama vile wakati wa tetemeko la ardhi Mkoani
Kagera imeweza kutoa mchango wake mkubwa kwa jamii na daima imekuwa ikilinda
maadili na weledi wa kazi ya uandishi kwa wafanyakazi wake jambo ambalo
linaonyesha ushirikiano mzuri baina ya Serikali, Kampuni na jamii.
“Mimi nawapongeza na
kuwashukuru sana MCL kwakuwa mstari wa mbele katika kulinda maadili katika kazi
zenu, endeleeni kulinda maadili kwa kuhabarisha na kuielimisha jamii, sijaona
mkivunja maadili ya kazi zenu na hakika mnajijengea sifa nzuri kwa wengine”,
alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa, kwa
sasa kumeibuka wimbi kubwa la Waandishi wa habari (Makanjanja) ambao hawana
vyeti wala weledi wa kufanya kazi ya uandishi wa habari na hao wamekuwa kila
wakati wakirusha taarifa zisizo sahihi hususani katika mitandao ya kijamii
jambo ambalo Serikali haiwezi kulifumbia macho.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa MCL, Bw. Francis Nanai amesema kwamba lengo la kampuni hiyo kuja na
muonekano mpya wa gazeti hilo ni kuwapa ladha mpya wasomaji wake nchini kote,
na hiyo ni mara ya sita kwa gazeti hilo kubadilishwa muonekano wake tangu
kuanzishwa kwake mwaka 2001.
“Sisi kama wadau wa
michezo tumewasikiliza wasomaji wa gazeti letu na tukayafanyia kazi mawazo yao
na ndiyo maana tukaamua kuja na muonekano mpya wa gazeti hili ambao uko
kimataifa zaidi”, alisema Nanai.
Aliongeza kuwa,
gazeti hilo lilianzishwa na waandishi wa tatu mwaka 2001 na lilikuwa likitoa
nakala 3,000 kwa siku ambapo kwa sasa kuja kwa muonekano mpya wa gazeti hilo
kutaongeza idadi ya wasomaji tofauti ilivyokuwa mwanzo na idadi ya uchapishaji
imeongezeka hadi kufikia nakala 60,000 kwa siku.




0 Comments