Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Ummy Mwalimu (kushoto) akifungua bomba kuashiria kupokea kisima toka
kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali
Polycarp Pengo kulia
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam,
Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo (kulia) akikata utepe kuzindua kisma cha maji
mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam,
Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo (katikati) akisisitiza jambo kwa wageni
waalikwa wakati akikabidhi kisima kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (Kushoto) kwa ajili ya mahabusu ya watoto mapema hii leo
jijini Dar es Salaam, kulia ni Padre Timotheo Maganga Mkurugenzi wa Mashirika
ya Kipapa Dar es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (kushoto)
akisisitiza jambo kwa wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati akipokea kisima
toka kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali
Polycarp Pengo (katikati) kulia ni Padre Timotheo Maganga
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu (kushoto) akisisitiza jambo kwa wageni waalikwa wakati
akipokea kisima toka kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama
Kardinali Polycarp Pengo Mkuu (katikati) kulia ni Padre Timotheo Maganga
Picha na Eliphace Marwa - Maelezo
...............................
Na
Agness Moshi na Anthony Ishengoma- Maelezo
Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es
Salaam leo limekabidhi Kisima chenye thamani ya
Shilingi Milioni kumi na moja laki saba na themanini (Sh. 11,780,000/=) kwa
Serikali ili kutatua tatizo la maji katika Mahabusu ya Watoto iliyoko Upanga
jijini Dar es Salaam.
Akiongea katika hafla ya makabidhiano ya
Kisima hicho Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Kardinali
Polycarp Pengo amesema lengo kuu la Mchango wa Kanisa katika ujenzi wa Kisima
hicho ni kuonesha kuwa Kanisa haliko mbali na Serikali katika shughuli
mbalimbali za ujenzi wa Taifa.
Alisema Kanisa Katolitiki Tanzania linashirikiana na
serikali katika juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali itikadi
za kidini chama au kikabila ili kusudi wanapotoka kwenye vituo hivyo watambue
wamesaidiwa kutokana na mapenzi mema ya
kanisa hilo kwa watu wote.
Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema
ujenzi wa kisima hicho umesaidia serikali kupunguza gharama ya kulipia bili ya
maji ambayo kwa mwezi mmoja serikali ilikuwa inalipa Shilingi laki nne kwa
ajili ya matumizi ya maji katika mahabusu hiyo.
Waziri Ummy amesema kutokana na ujenzi wa kisima
hicho tatizo la maji limekwisha kwa asilimia
mia moja kwasababu kisima hicho kina uwezo wa kuzalisha lita 5,000 kwa
saa.
Aidha amesema kuwa fedha ambazo
zimeokolewa na ujenzi wa kisima hicho zitatumika kwa ajili ya kuwakatia Bima ya
Afya Watoto wanaozuiliwa katika vituo hivyo ili kuwahakikishia upatikanaji wa
matibabu.
Amesema ni muhimu kwa jamii kufahamu kuwa
ni Mahakama tu ndio yenye uwezo
wa kutoa amri ya watoto kuhifadhiwa katika
mahabusu hiyo na sio mtu au
chombo chochote kingine.
Waziri Ummy alimwambia Kardinali Pengo
kuwa hapa nchini kuna Mahabusu 5 ambazo ni Mahabusu ya Watoto Dar es Salaam
(Upanga), Mahabusu ya Watoto Tanga, Mahabusu ya Watoto Moshi, Mahabusu ya
Watoto Arusha na Mahabusu ya watoto Mbeya.
Amezitaja huduma zinazotolewa na Wizara yake kwa watoto walioko
kwenye Mahabusu hizo kuwa ziko za aina tatu ambazo ni uhifadhi na utunzaji wa watoto, huduma za maadilisho kwa watoto ambao
tayari Mahakama imewahukumu, na huduma za Kijamii za Marekebisho ya tabia kwa
watoto waliokinzana na Sheria.
Wakati huo Mkurugenzi wa Mashirika ya
Kipapa Kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni
Mwakilishi wa watoto na vijana wainjilishaji mtandaoni Padre Thimotheo
Nyasulu amesema kuwa, wameamua kutoa
msaada huo baada ya kuona changamoto hiyo walipotembelea kituo hicho Desemba ,2016
kama sehemu ya matendo ya huruma kwa kanisa.
Aidha Padre Nyasulu ametoa rai kwa
Wananchi na waandishi wa habari kutoendelea kuita vituo vya watoto waliokinzana
na Sheria Mahabusu na kushauri viitwe vituo vya malezi kwasababu hali hiyo
inawafanya kujiona wametengwa hali inayowaongezea adhabu.
Waziri Ummy alisema
Mahabusu za watoto ni moja kati ya huduma kongwe hapa nchini mahususi kwa kuwahifadhi watoto walio kinzana na Sheria na
ambao kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kupata dhamana kwa kesi au mashauri ambayo yanawakabili Mahakamani.





0 Comments