Maafisa karibu 3,000 wa idara ya kulinda bahari wanasaidia katika uokoaji Houston na viunga vyake.
Watu takriban 2,000 wameokolewa
kutoka kwa mafuriko katika mji wa Houston na viunga vyake, huku kimbunga
Harvey kikiendelea kusababisha mvua kubwa sana maeneo ya jimbo la
Texas.
Kumekuwa na ripoti za kutokea kwa vifo pamoja na magari kadha kuzidiwa na nguvu za maji.
Hata hivyo, uchunguzi bado unaendelea, afisi ya liwali mkuu wa wilaya ya Harris, Darryl Coleman amesema.
Gavana wa Texas Greg Abbott ameambia wanahabari kwamba hawezi kuthibitisha vifo vinavyodaiwa kutokana na mafuriko hayo.
Idara ya Taifa ya Hali ya Hewa (NWS) imesema hali ambayo inashuhudiwa katika eneo hilo haijawahi kushuhudiwa awali.
Idara hiyo imesema kulitokea mafuriko ya ghafla eneo la katikati mwa mji wa Houston, na uchukuzi umetatizika.
Vyumba vingi vya kutoa hifadhi wakati wa majanga vimefunguliwa, ukiwemo ukumbi mmoja wa mikutano.
Gavana
Abbot amesema barabara karibu 250 zimefungwa Texas na kwamba ameiomba
serikali kuu itangaze janga katika wilaya 19, ombi ambalo limeidhinishwa
na Rais Donald Trump.
"Tutaendelea kupokea mvua kubwa," amesema gavana huyo.
NWS awali walisema walikuwa wamepokea taarifa za vifo vitano, lakini
wamesema wameweza kuthibitisha kifo cha mtu mmoja pekee eneo la Houston.
Kufikia
sasa, watu wawili wamethibitishwa kufariki tangu kimbunga hicho
kilichofika maeneo ya bara, katika wilaya ya Aransas, ambapo Rockport
ndio mji mkuu, mtu mmoja alifariki baada ya nyumba yake kushika moto
Ijumaa usiku.
Na eneo la Houston, mwanamke mmoja alifariki akiendesha gari katika barabara zilizokuwa zimefurika maji Jumamosi.
Meya
wa Houston Sylvester Turner amewashauri wakazi kutopigia simu maafisa
wa huduma za dharura ila tu iwapo maisha yao yanatishiwa na wanahitaji
kuokolewa kwa dharura.
"Msiingie barabarani. Msifikirie kwamba kimbunga kimepita," amesema.
Mjini
Washington, ikulu ya White House imesema Rais Trump atazuru Texas
Jumanne kutathmini uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho.
Bw
trump alikuwa amesema awali kwamba angezuru eneo hilo haraka
iwezekanavyo lakini kwa kuhakikisha kwamba hatatatiza juhudi za uokoaji.
Maafisa wa hali ya hewa wamesema vifo vingi hutokea magari yanaposombwa na maji.
Houston ni moja ya miji yenye watu wengi zaidi Marekani
Kufikia saa nane adhuhuri saa za Texas Jumapili, NWS walisema mji wa
Houston ulikuwa umeandikisha mvua ya kina cha sentimeta 64.8 (inchi
25.50) kwa mwezi Agosti, na kuufanya kuwa mwezi wenye mvua kubwa zaidi
katika historia ya mji huo.


























0 Comments