Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan akisisitiza jambo kwa kina mama (hawapo
pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Kiuchumi kwa
Kinamama Mkoa wa Dar es Salaam katika viwanja vya TTCL Kijitonyama leo.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na
Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Kiuchumi kwa Kinamama Mkoa wa Dar es Salaam
Mhe. Sophia Mjema akisisitiza jambo kwa kina mama (hawapo pichani) wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Jukwaa hilo iliyofanyika katika viwanja vya TTCL
Kijitonyama leo.
Baadhi ya kina mama wakifurahia jambo wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Kiuchumi kwa Kinamama Mkoa wa Dar es
Salaam iliyofanyika katika viwanja vya TTCL Kijitonyama leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mama Samia Suluhu akikata utepe wa mfano wa hundi wakati wa hafla ya
uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Kiuchumi kwa Kinamama Mkoa wa Dar es Salaam katika
viwanja vya TTCL Kijitonyama leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mama Samia Suluhu (kushoto) akipokea hundi toka kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei wakati wa hafla ya uzinduzi wa
Jukwaa la Uwezeshaji Kiuchumi kwa Kinamama Mkoa wa Dar es Salaam iliyofanyika
katika viwanja vya TTCL Kijitonyama leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mama Samia Suluhu (katikati) akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi
milioni ishirini kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Kiuchumi kwa Kinamama
Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Sophia Mjema (kushoto) na kulia ni Mwenekiti wa
Baraza la Wafanyabiashara Wanawake Bi. Jackline Maleko, mapema hii leo wakati
wa hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Kiuchumi kwa Kinamama Mkoa wa Dar
es Salaam.
Picha
na: Eliphace Marwa.
.......................
Na: Ismail Ngayonga, MAELEZO
DAR ES SALAAM
MAKAMU
wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake nchini kuchangamkia fursa ya
uanzishaji wa majukwaa ya kiuchumi ili waweze kuunganisha nguvu katika
upatikanaji wa masoko, mitaji, na elimu ya ujasiriamali hatua itakayowasaidia kupiga
hatua kubwa na haraka za maendeleo.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa Jukwaa la Kuwezesha Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Dar es Salaam leo
(Agosti 26, 2017) Jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais amesema siri kubwa ya
kuinua hali za kiuchumi kwa mwanamke, ni wanawake wenyewe kuweka nguvu za
kufikiri na mipango thabiti.
Aliongeza kuwa muda
umefika wa kuwakukomboa wanawake kutoka katika lindi la umaskini linalotokana
na kutowezeshwa kiuchumi, na hilo litawezekana kwa kuwapa ujuzi na maarifa,
kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu na kwa urahisi pamoja na kuweka
mifumo ya kisheria itayopiga vita mila kandamizi.
“Nimefarijika kusikia
kuwa mpaka leo hii ukijumuisha na jukwaa hili la Dar es Salaam tuna majukwaa 23
ya Mikoa, 105 ya Halmashauri, 236 ya Kata, nitoe rai kwa mikoa ya Dodoma,
Njombe na Ruvuma kuhakikisha kuwa inaanzisha haraka majukwaa hayo” amesema Mhe.
Samia.
Aidha Makamu wa Rais
alisisitiza kuwa ni vyema uwepo utaratibu wa kutembelea majukwaa hayo ili
kuweza kubadilishana uzoefu sambamba na kusambaza fursa zinazojitokeza katika
majukwaa ya vijijini ili kuhakikisha kuwa kila mwanamke Mtanzania ananufaika na
keki ya taifa.
Kwa mujibu wa Mh Samia,
ajenda mpya ya malengo ya maendeleo endelevu imeazimia kukamilisha yote
yaliyokuwa hayajatekelezwa katika malengo ya maendeleo ya millennia na
kuhakikisha kuwa ifikapo ukomo wa utekelezaji wa ajenda ya malengo ya maendeleo
endelevu mwaka 2030, usawa wa mwanamke utakuwa umefikia asilimia 50 kwa 50.
Katika hotuba yake
hiyo Mhe. Samia alitoa wito kwa washiriki kulitumia vyema jukwaa hilo ili
waweze kujipanga na kujikomboa kiuchumi kwa kuhakikisha wanaijenga Tanzania
mpya ya viwanda kwa kujishughulisha na uzalishaji wa mazao ya kilimo ambayo
ndio malighafi kuu ya kuendesha viwanda hivyo.
“Muda umefika sasa wa
kuhakikisha kuwa hamtambuliki tu kwa ‘mwanamke jiko’ bali mwanamke ‘viwanda’,
hapa namaanisha mwanamke mwenye maamuzi yake kiuchumi, kielimu, kibiashara,
kisiasa na mwenye uwezo wa kushika nyadhifa mbalimbali” amesema Makamu wa Rais.
Akizungumza katika
uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei amebainisha
kuwa kati ya asilimia 17 ya watanzania wanaotumia huduma rasmi za kibenki,
wanawake ambao ni asilimia 52 ya watanzania milioni 56 wanaotumia huduma rasmi
ya kibenki ni asilimia 10.1 tu kati ya watanzania wanaotumia huduma za kibenki.
Dkt. Kimei anasema
kupitia jukwaa, hilo Benki hiyo imeweza kuzindua rasmi huduma ijulikanayo
SIMAccount, ambayo inatoa fursa kwa wateja kuwa na uwezo wa kufungua akaunti za
vikundi, hatua ambayo itaweza kutoa suluhisho la utunzaji wa fedha kwa wanawake
na wanaume ikiwemo kuangalia miamala na kumbukumbu.
“Kupitia huduma ya
SIMAccount, kinamama watakuwa na uwezo wa kufungua akaunti ya kikundi na
kuwaunganisha wenzao mtandaoni bila ulazima wa kukutana, kama yalivyo makundi
maarufu ya What’sup” amesema Dkt. Kimei.
Kwa mujibu wa Dkt.
Kimei kwa wateja wapya ambao simu zao bado hazipo katika mfumo, watatakiwa
kukamilisha usajili wao kupitia tawi la benki hiyo au kupitia wakala wa fahari
huduma ambao kwa sasa wapo zaidi ya 2,500 nchi nzima.
Alisisitiza kuwa huduma
hiyo ya SIMAccount itakuwa suluhisho la kipekee kwa wanawake na Watanzania kwa
ujumla kwa kuwa itawezesha kufungua akaunti zao za vikundi pale walipo,
kujiunga wenyewe na kutengeneza miundombinu ya kukopeshana wenyewe.






0 Comments