Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura alipokuwa
akijibu maswali leo Bubgeni
Mjini
Dodoma.
(Picha na Daudi
Manongi, MAELEZO, Dodoma)
...
Na Eleuteri Mangi,
WHUSM, Dodoma
Halmashauri zote
nchini zimetakiwa kuendeleza na kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli
za michezo na burudani ili kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo
yao inazingatiwa.
Wito huo umetolewa
leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Mhe. Anastazia Wambura alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilolo Venance
Mwamoto lililohoji Serikali imechukua hatua gani kuhusu timu ya taifa kuendelea
kufanya vibaya katika michezo ya Kimataifa.
“Serikali inaendelea
kufanya juhudi za kuendeleza michezo nchini ili kuwa na timu bora za michezo
katika ngazi mbalimbali hasa ngazi ya taifa”amesema Mhe.Anastazia
Aidha alizitaja
juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuendeleza michezo ni pamoja na kutoa na
kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa wataalamu wa michezo wakiwemo Waalimu na
Maafisa michezo kwa ngazi za Wilaya na Mikoa kupitia Baraza la Michezo la Taifa
na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Naibu Waziri Wambura
ameongeza kuwa juhudi nyingine zinazoendelea kufanywa na Serikali ni kuboresha
mazingira ili wadau wa michezo wawekeze Kisayansi katika michezo kuanzia umri
mdogo kwa lengo la kugundua na kukuza vipaji na hatimaye kupata wachezaj mahiri
wa timu za Taifa.
Hatua nyingine ni
kutenga shule mbili maalum za michezo kwa kila Mkoa pamoja na kuhamasisha wadau kuanzisha shule za aina
hiyo, kutoa ushauri elekezi kwa Vyama vya Michezo wakati wa maandalizi ya timu
za Taifa zinazoshiriki kwenye michezo ya Kimataifa ikiwemo Olimpiki, Michezo ya
Afrika na Michezo ya Jumuiya ya Madola, kuendesha na kuratibu mashindano ya
michezo kwa ajili ya wanafunzi wa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na michezo ya
Shule za Sekondari (UMISSETA) kwa kushirikiana na Wizara nyingine.
Kwa upande wa uwepo
wa wachezaji wengi wa Kimataifa wanaochezea timu za hapa nchini, Naibu Waziri
amesema kuna wachezaji 40 wa kigeni wanaocheza mpira nchini wakati wachezaji wa
Kitanzania wanaocheza mpira nje ya nchi idadi yao ni 14 huku akisisitiza kuwa
Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo ambapo kuanzia mwezi Julai mwaka
huu fedha zimeanza kupelekwa Baraza la Michezo la Tifa (BMT) ili ziweze
kutumika katika kusimamia na kuendeleza michezo nchini.
Akijibu swali la
nyongeza la Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay alilouliza kuhusu
uendelezwaji wa Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti
Boys) ambao walionesha uwezo mkubwa katika mashindano ya Kimataifa mwaka huu,
Naibu Waziri Wambura amesema kuwa hadi sasa vijana hao wanalelewa, kutunzwa na
kuendelezwa katika kituo cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili baadae waweze
kutumika katika timu za wakubwa kwa manufaa ya taifa.
Ili taifa lifanikiwe
katika sekta ya michezo, Wabunge wanawajibu wa kushiriki kikamilifu katika
shughuli za maendeleo ya michezo katika maeneo yao ikiwemo uibuaji wa vipaji na
ujenzi wa miundombinu kwa kuhamasisha wadau mbalimbali.

0 Comments