Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba.
....
Na: Lilian Lundo,MAELEZO-Dodoma
Serikali imesema kila Mtanzania anajukumu la kuhifadhi
Tabaka la Ozoni kwa kutotumia bidhaa zenye madhara kwa Tabaka hilo
katika biashara na shughuli za kila siku za majumbani.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira January Makamba kupitia taarifa aliyoitoa leo, kwa
vyombo vya habari juu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la
Ozoni inayofanyika kila mwaka, Septemba 16.
"Kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu ni muhimu
tuzingatie kwamba juhudi za kila mmoja wetu zinatakiwa ili kupunguza na
kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na bidhaa
tunazonunua na kutumia majumbani au sehemu za biashara ," amefafanua
Makamba kupitia taarifa hiyo.
Makamba amesema kuwa kila mwananchi anatakiwa kuepuka
kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi
haribifu kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwisha tumika (mitumba)
na ambavyo vinatumia vipoozi aina ya Chlorofluorocarbons (R11 na R12).
Vile vile amewataka Watanzania kununua bidhaa zilizowekwa
nembo rasmi isemayo "Ozone friendly" ikiashiria haina wala
haikutengenezwa na kemikali zinazomong'onyoa Tabata la Ozoni.
Aidha amewaasa Watanzania kuepuka kutupa hovyo majokofu ya
zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong'onyoa Tabaka
la Ozoni aina ya " CFCs" na "halon". Ila wanapotaka kutupa wanatakiwa
kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mafundi ama mamlaka zinazohusika.
Pia mafundi wa majokofu na viyoyozi wametakiwa kuhakikisha
kuwa wananasa na kutumia tena vipoozi kutoka kwenye viyoyozi na majokofu
wanayohudumia badala ya kuviacha huru visambae angani.
Mafundi hao wanatakiwa kutoa elimu kwa wateja wao kuhusu
njia rahisi ya kutambua uvujaji wa vipoozi kutoka katika majokofu na
viyoyozi wavyotumia.
Kitaifa, maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya
Tabaka la Ozoni yatafanyika kwa njia ya uelimishaji Umma kuhusu Tabaka
la Ozoni, faida zake, madhara ya kuharibika kwa Tabaka hilo na matumizi
salama ya bidhaa zenye kemikali rafiki kwa Tabaka hilo.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika kuadhimisha siku hiyo ni
"Kutunza na Kulinda Viumbe Hai Duniani" ( Caring for All Life Under the
Sun).

0 Comments