Makamu wa Pili wa Rais
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (wa pili kulia)
akioneshwa Mfumo wa kukusanya Mapato wa Kielektroniki uliopo Kituo cha Taifa
cha Data, Dar es Salaam na mtaalamu wa umeme na mifumo ya upozaji wa Kituo
hicho Bwana. Deus Lwabukuna.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (aliyesimama)
akifafanua jambo kuhusu utayari wa taasisi za Serikali yake kutumia Kituo cha
Taifa cha Data kilichopo Dar es Salaam. Anayesikiliza wa kwanza kushoto ni
Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Eng.
Maria Sasabo na wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu wa TTCL Bwana Waziri Waziri
Kindamba.
Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Moshi Kakoso (aliyesimama)
akichangia jambo kuhusu matumizi ya Kituo cha Taifa cha Data wakati wa ziara ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Seif
Ali Iddi (hayupo pichani) alipotembelea kituo hicho Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Eng. Omary Nundu (aliyesimama) akisisitiza
jambo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (hayupo pichani) alipotembelea kituo cha
Taifa cha Data kilichopo Dar es Salaam.
Muonekano wa Mfumo wa
Kukusanya Mapato wa Kielektroniki (electronic Revenue Collections System –
eRCS) uliopo kwenye Kituo cha Taifa cha Data kilichopo Dar es Salaam.
...
Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imevutiwa na utendaji kazi wa Kituo cha Taifa cha Data (National
Internet Data Centre-NIDC) kwa kukusanya mapato ya Serikali kwa kutumia Mfumo
wa Kukusanya Mapato wa Kieletroniki (eRCS – electronic Revenue Collections
System)hivyo kuongeza mapato ya Serikali ya Muungano ya Tanzania na Mapinduzi
ya Zanzibar.
Hayo yameelezwa leo na
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Seif
Ali Iddi alipotembelea Kituo cha Taifa cha Data kilichopo Dar es Salaam. Katika
ziara hiyo, Balozi Iddi amevutiwa na kuridhishwa na utendaji kazi wa Kituo
hicho ambapo kinatumia Mfumo wa Kukusanya Mapato wa Kielektroniki ambao
umeunganisha taasisi za Serikali na sekta binafsi. “Zanzibar tunategemea sekta
ya utalii kuongeza mapato yetu, wadau wote wa sekta hii wajiunge na mfumo huu
pamoja na taasisi zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili tuweze kuona
makusanyo ya mapato yetu kwa wakati, ufanisi na kwa uhakika”, amesema Balozi
Iddi. Mhe. Balozi Iddi ameongeza kuwa Mfumo huu unasaidia kukusanya mapato ya
Serikali, Serikali inataka kuwatumikia wananchi wake na kuwaletea maendeleo na
hakuna Serikali yoyote inayoweza kufanya hayo bila ya kodi.
Katibu Mkuu wa Mawasiliano,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Eng.
Maria Sasabo ambaye
amemuwakilisha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
amesema kuwa Serikali ya Muungano wa Tanzania tayari inashirikiana na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mfumo huu kukusanya na kuongeza mapato ya
Serikali ambapo yatawezesha Serikali zetu kuhudumia wananchi wake katika nyanja
ya afya, elimu, miundombinu, maji, barabara na kilimo cha kisasa.
Mtendaji Mkuu wa
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Bwana Waziri Waziri Kindamba amesema kuwa Mfumo
huo umetengenezwa na wataalamu wazalendo wa watanzania wakishirikiana kwa
pamoja kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na wanahusika katika uendeshaji wa Mfumo huo.
Pia,
ameongeza kuwa taasisi za Serikali na sekta binafsi zitumia Mfumo huo na hadi
hivi sasa jumla ya Kampuni saba za mawasiliano na benki kumi na nne
zimeunganishwa kwenye Mfumo huo na makusanyo ya mapato yao yanapita na
kuonekana kwenye Mfumo huo. Bwana Kindamba amesema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar
imeweza kuongeza makusanyo ya mapato yake kutoka shilingi milioni kumi na tatu
hadi milioni mia tano kwa mwezi kupitia Mfumo huo tangu ulipoanza rasmi
kutumika ulipozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli mwezi Juni mwaka huu hadi Agosti mwaka huu.
Naye Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Moshi Kakoso ameiomba Kampuni
ya Simu Tanzania (TTCL) kufanya kazi kibiashara zaidi na kwa faida na sio kwa
mazoea kama hapo awali.
Vile vile Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Eng. Omary Nundu
amesema kuwa azma ya Bodi yake ni kuhakikisha kuwa TTCL inaendelea kutoa huduma
za mawasiliano kwa wananchi nchi nzima na ameiomba Serikali kuendelea kuiunga mkono
kampuni kongwe ya kizalendo, TTCL ili iweze kujiendesha kwa faida.
Kituo cha Taifa cha
Data kimejengwa na Serikali ya Muungano ya Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano kuanzia mwaka 2014 na kukamilika mwaka 2015 kwa gharama
ya dola za marekani milioni thelathini na tano na ni cha kiwango cha kimataifa.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano





0 Comments