Wafanyakazi
wa Mamlaka ya Bandari nchini wakiendelea na zoezi la upakiaji wa mbolea ya
kupandia tani elfu 23 tayari kwenda kwa wakulima mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi
wa Mamlaka ya Bandari nchini wakiendelea na zoezi la kufunga mbolea ya kupandia
katika mifuko tayari kwa kupakiwa na kusafirishwa kwenda kwa wakulima.
Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya
Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania(TFRA) Bw. Lazaro Kitandu (katikati)
akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati zoezi la upakuaji wa mbolea ya
kupandia ukiendelea katika bandari ya Dar es Salaam mapema hii leo.
Picha na Eliphace Marwa - Maelezo
...
Na. Eliphace Marwa - Maelezo
Serikali imeingiza nchini jumla
ya tani elfu 32 za mbolea ya kukuzia pamoja na tani elfu 23 za mbolea ya
kupandia kupitia mfumo mpya wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja, lengo likiwa ni
kudhibiti bei kwa kuzingatia bei elekezi.
Akizungumza na waandishi wa
habari Jijini Dar es Salaam wakati zoezi la upakuaji wa mbolea hiyo likiendelea
Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya
Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania(TFRA) Bw. Lazaro Kitandu amesema kuwa
mpaka sasa jumla ya tani elfu 55 za mbolea zimewasili nchini.
Hii ni awamu ya kwanza ya
kuingiza mbolea nchini kupitia mfumo mpya ya uagizaji mbolea kwapamoja ambapo
kampuni ya OCP S.A ya nchini Morocco imeingiza jumla ya tani elfu 23 za mbolea
ya kupandia na Kampuni ya Premium Agro Chem imeingiza tani elfu 32 za mbolea ya
kukuzia.
“Mpaka sasa zoezi la kupakua mbolea ya kupandia (DAP) tani elfu 23
linaendelea vizuri na mara baada ya kumaliza kupakua mbolea hii tutaanza zoezi
la kupakua mbolea ya kukuzia (UREA) ambayo ni tani elfu 32,” alisema Bw.
Kitandu.
Kitandu aliongeza kuwa Mheshimiwa
Waziri wa kilimo juzi alipokuwa anaongea na waandishi wa habari mjini Dodoma na
akasisitiza bei ambazo zimetolewa zisimamiwe na kila ngazi kwasababu taasisi
peke yake haiwezi kuwa na watu kila mahali hivyo Tawala za mikoa, Serikali za
mitaa mpaka Kijiji zitasaidia kusimamia bei ambazo zimetolewa.
Pia Kitandu aliongeza kuwa
kuhusiana suala la bei ya mbolea hiyo itatangazwa kupitia vyombo vya habari
kama vile magazeti na televisheni na hivyo kutoa onyo kwa mawakala kujipangia
bei kwa kuuza mbolea nje ya bei
elekezi ya Serikali kwamba watachukuliwa hatua za kisheria kama kunyang’anywa
leseni, kufungwa, faini au vyote kwa pamoja.
Aidha Kitandu alisisitiza
kuwa mbolea hizi siyo mbolea za ruzuku kwani wakulima wengi wamekuwa
wakichanganya mbolea hizi na mbolea za ruzuku na amefafanua kuwa mbolea hii
imefanyiwa utaratibu wa kudhibiti toka kule inapotoka na hivyo serikali
itahakikisha mbolea hii inauzwa kwa kulingana na bei ya soko la dunia.
Aidha Bw. Kitandu aliwahakikishia wakulima kuwa mbolea
itasafirishwa mpaka vijijini kwa kutumia treni na malori kwa sehemu ambapo treni
haiwezi kufika, na amewatoa hofu wakulima kuwa msimu unaoanza mwezi huu
wameingiza tani 23,000 kwa mbolea ya kupandia (DAP) na tani 32,000 kwa mbolea
ya kukuzia (UREA) ambapo watakuwa wanaagiza kwa awamu kwa miezi miwili miwili.




0 Comments