Na.Paschal Dotto
-Maelezo.
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali
inaendelea kuhakikisha Mahakama hazijihusishi na vitendo vya rushwa ili kutoa
haki kwa mujibu wa Sheria.
Mh. Samia ameyasema
hayo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa Chama cha majaji na
mahakimu wa nchi za Jumuiya ya Madola uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya
Tanzania.
‘Ninaamini, nia ya
kujenga mahakama bora na yenye kuaminika kwa Tanzania haiwezi kutenganishwa na
juhudi za serikali katika kuondoa umaskini na rushwa” amesisitiza Mh.Samia.
Aidha Makamu wa rais
amesema kuwa kuna uhitaji mkubwa kwa nchi kuwa na mahakama huru, makini na
yenye kuwajibika ipasavyo kwani mahakama huru ni msingi mzuri wa demokrasia.
Alisema kuwa pamoja na
changamoto mbalimbali za mahakama uhuru wa mahakama ambao ni umakini,uwajibikaji na utoaji haki
kwa kufuata utawala wa sheria kwa wananchi wake uko palepale.
Kwa upande wa Tanzania Mhe.
Samia amesema kuwa katika awamu ya tatu ya mapambano dhidi ya rushwa ambapo kwa
awamu mbili zilizopita serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza
malalamiko yaliyotokana na ukiukwaji wa haki.
Katika awamu ya tatu ya
mkakati wa kupambana na rushwa utakaochukua miaka mitano kuanzia 2017 hadi 2022,
Tanzania itachukua uzoefu kutoka kwenye mkuatno huu wa kimataifa kutoka kwa
nchi wanachama wa Jumuiya ya madola.
Kwa upande wake Jaji
mkuu wa Tanzania Professa Ibrahim Juma alisema mahakama hiyo iko huru na
inatekeleza majukumu yake pasipo kuingiliwa na mtu yeyote na akaahidi kuendelea
kubadilishana uzoefu na mahakama za nchi wanachama ili kuboresha utendaji kazi.
Aidha Profesa Juma
amesema Mahakama ya Tanzania kupitia majaji imekubaliana kuwa kila Jaji atatakiwa
kuhukumu zaidi ya kesi 220 ambazo ni asilimia 38 ya kesi zilizoahirishwa mwaka
2012 hadi asilimia 5 Desemba 2016 na hii itafanyika kila mwaka ili kujipima wao
wenyewe kama moja ya malengo waliyojiwekea.
Akizungumzia mipango ya
mahakama hiyo Profesa Juma amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2020 mahakama hiyo
itakuwa imekamilisha ujenzi wa mahakama
Kuu 13,mahakama za hakimu mkazi 14,mahakama za Wilaya 48,pamoja na mahakama za
Mwanzo 100.
Mkutano wa mwaka huu wa chama cha majaji na
mahakimu wa nchi za jumuiya ya madola umefanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini
tangu Tanzania ijiunge na chama hicho mwaka 1970.

0 Comments