Katibu
Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel
(aliyevaa kaunda) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo leo mjini Dodoma ambapo awali ndiye alikuwa
anaiongoza kabla ya mabadiliko ya safu ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu
Wakuu yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli Alhamisi tarehe 26 Oktoba, 2017.
(Picha na Eleuteri
Mangi-WHUSM, Dodoma)
..........
Na Eleuteri Mangi,
WHUSM, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel amewaaga watumishi wa
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo leo mjini Dodoma.
Prof. Elisante awali
ndiye alikuwa anaiongoza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla ya
mabadiliko ya safu ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu yaliyofanywa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Alhamisi Oktoba
26, 2017.
Prof. Elisante
amewashukuru watumishi hao kwa ushirikiano waliompatia tangu alipoingia
Wizarani hapo Aprili 01, 2012 akiwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana,
Naibu Katibu Mkuu na baadae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo. Idara ya Maendeleo ya Vijana
kwa sasa ipo Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Tunapimwa kwa
utendaji kazi, endelezeni utamaduni wa kuchapa kazi kwa kujituma, kushirikiana,
kupendana na kuwajali watumishi wote hasa wa ngazi za chini” alisisitiza Prof.
Elisante.
Aidha, amewataka
watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa wabunifu ili
utendaji kazi wao uwe wenye tija kwa wananchi wote watakao kuja kupata huduma
wizarani hapo.
Kwa upande wa
watumishi wa Wizara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Maedeleo ya Utamaduni Bi. Lilly
Beleko amemhakikishia Prof. Elisante kuwa wataendelea kutumia fursa zilizopo
kwa maedeleo ya Wizara na taifa kwa ujumla kwa kutumia ujuzi walionao kulingana
na taaluma zao.
Naye Mkurugenzi wa Sera
na Mipango Petro Lyatuu amesema watamkumbuka Prof. Elisante kwa utendaji wake
wa kazi kwa kujali muda, kila mara na alikuwa akiwasisitiza kutumia simu
kimkakati kwa kupokea na kujibu simu ambapo kila mara alikuwa akisisitiza “Simu
zenu mziweke kimkakati wakati wote”.
Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo sasa inaongozwa na viongozi wapya ambapo Katibu
Mkuu wake ni Bi. Suzan Paul Mlawi na Naibu Katibu Mkuu akiwa Nicholaus B.
William.


0 Comments