
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wana-Lindi na wana-Ruangwa watumie fursa zilizopo ili kufanikisha maandalizi ya sherehe za Maulid na Baraza la Maulid Kitaifa mwaka huu.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Novemba 5, 2017)
wakati akizungumza na viongozi wa dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Lindi na wilaya
ya Ruangwa mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.
Waziri Mkuu amesema sherehe hizo zitafanyika
Desemba mosi kwa mkesha wa Maulid na kufuatiwa na Baraza la Maulid
litakalofanyika Desemba 2, saa 3 asubuhi kwenye viwanja vya shule ya msingi Likangale.
Aliwataka wana-Ruangwa waharakishe kujenga nyumba
za kulala wageni na sehemu za kula ili waweze kupokea ugeni huo mkubwa wa
kitaifa. “Kila mmoja anayeona hapo kuna fursa, ni lazima aitumie vizuri,”
alisisitiza.
“Kwa niaba ya wana-Ruangwa, tunamshukuru Mheshimiwa
Mufti na Baraza la Maulamaa kwa kuridhia sherehe hizi zifanyike kitaifa hapa
wilayani kwetu. Nitumie fursa hii kuwaomba Waislamu wote tuungane katika
sherehe hizi licha ya tofauti za madhehebu yetu tuliyonayo,” alisema.
Alisema uamuzi huo wa BAKWATA ulitangazwa kwenye
Baraza la Maulid lililofanyika Singida, mwaka jana ya kwamba wameamua
kuadhimisha sherehe hizo kwenye ngazi ya wilaya badala ya kuwa inafanyika makao
makuu kila mwaka.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaarifu viongozi
hao kwamba maandalizi yanaendelea na kwamba vifaa mbalimbali kama mchele, vitoweo,
unga wa ngano, sukari, maji, juisi, mahema, mikeka na mazulia vimekwishapatikana.
“Ninaomba Kamati ya Uhamasishaji iifanye kazi hii
kwa kutambua kuwa jambo hili si la kwenu peke yenu, bali linaungwa mkono na
Serikali, na hii ni kwa sababu Serikali yenu inafanya kazi kwa karibu sana na
viongozi wa dini,” alisema.
Alisema misingi ya amani katika nchi hii imejengwa
na mahubiri ya viongozi wa dini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji, Sheikh Ali Mohammed Mtopa
alisema Ruagwa iko tayari na imepokea wito huo wa kitaifa. “Tunakuhakikishia
wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wawakilishi wa Mufti waliopo hapa kwamba
tumepokea hiyo heshima,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Itifaki kutoka BAKWATA Makao
Makuu na Msimamizi wa Malidi za Kitaifa, Sheikh Mohammad Nassir ambaye alisema
wana Ruangwa an wana Lindi wanalo jukumu la kuhamasisha watu washiriki sherehe
hizo.
“Hamasa haitatoka Morogoro au Dar es Salaam bali
hapahapa Lindi. Tunataraji watu wasiopungua 10,000 watahudhuria sherehe hizi za
Maulid kutoka wilaya zote za mkoa wa Lindi na hii ni mbali wawakilishi kutoka
kila mkoa wapatao 100 -150,” alisema.
Waziri Mkuu anatembelea vijiji vya jimboni mwake
ambako atahutubia wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, NOVEMBA 5, 2017.
0 Comments