Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia
wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi jengo la ofisi ya Taifa ya
Takwimu mjini Dodoma leo Desemba 20, 2017
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa onyo
kwa wale wote wanaotoa takwimu za upotoshaji kuacha mara moja na
kuzitaka mamlaka husika kuwachukulia hatua.
Rais
Magufuli ametoa onyo hilo leo mjini Dodoma wakati wa uwekaji jiwe la
msingi la jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dodoma.
“Watanzania
mfuate takwimu zinazotolewa na vyombo husika,ukitaka takwimu zozote
nendeni kwa wataalamu na wahusika wanaotoa takwimu sahihi kwa sababu
ukikosea kutoa takwimu sahihi umeichafua nchi” ameongeza Dkt. Magufuli.
Dkt
Magufuli ameongeza kuwa takwimu ni muhimu katika Nyanja zote ikiwemo
kusaidia kupanga mipango ya maendeleo ya nchi ambapo husaidia kuweka
malengo, kupanga malengo na pia kuliwezesha taifa kujipima kiasi gani
imefikia maendeleo.
Aidha,akizungumzia
hali ya ukuaji wa uchumi nchini Dkt Magufuli amesema kuwa katika nusu
ya mwaka huu uchumi umekuwa kwa asilimia 6.8 ambao umepelekea kuongoza
kwa nchi za Afrika Mashariki na kuwa miongoni mwa nchi za Afrika ambapo
uchumi wake unaokuwa kwa kasi.
Wakati
huo huo, Dkt Magufuli amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango kufuatilia
Kampuni ya Airtel kujua ukweli ya kwamba Kampuni hiyo ni sehemu ya
Kampuni ya TTCL.
Mbali na hayo Dkt. Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia, Serikali ya Canada na Shirika la misaada la Uingereza
(DFID) kwa misaada wanayoendelea kuipatia nchi na kuwaahidi kuwa kila
senti ya msaada itakayotolewa na mashirika hayo itatumika ipasavyo.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) amesema
kuwa Tanzania imekuwa nchi ya pili barani Afrika baada ya Afrika Kusini
katika utoaji wa Takwimu bora kati ya nchi 54 ikiwa ni tathimini ya
Benki ya Dunia mwaka 2016.
“Tumeendelea
kutoa mafunzo kwa wanatakwimu katika taasisi za Serikali, Idara na
Wizara ili kuendana na mabadiliko katika eneo la takwimu” ameongeza Dkt.
Chuwa.
Nae
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango ameongeza kuwa ujenzi wa
jengo hilo ni matokeo ya agizo la uhamasishaji wa Serikali kuhamia Makao
Makuu ya nchi Dodoma.
“Ujenzi
wa jengo hili unagharimu shilingi Bilioni 11.6 mpaka kukamilika kwakwe
na pia ujenzi umetoa ajira za muda wa wastani kwa vijana 120 kila siku
huku asilimia 100 ya vifaa vinavyotumika katika jengo hili ni vifaa
kutoka ndani ya nchi, ujenzi wa jengo hili unatarajiwa kumalizika mwezi
Januari, 2018” amefafanua Dkt. Mpango.
Pia
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bella Bird ameipongeza Ofisi ya
Taifa ya Takwimu kwa kuwa miongozi mwa Ofisi bora katika utoaji wa
takwimu.
“Tanzania
imefanya maendeleo makubwa katika uhifadhi wa takwimu, hivyo Benki ya
Dunia itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Takwimu ili kuweka
mifumo thabiti ya kukuza uchumi wa viwanda” amefafanua Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia
kuhusu upotoshaji wa takwimu hasa kwa vyombo vya habari nchini,
Mkurugenzi Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas
amevitaka vyombo vya habari na wanahabari nchini kuhakikisha wanatumia
takwimu sahihi na zinazotoka katika vyombo sahihi ili kuendeleza weledi
wa taaluma.

0 Comments