Na. Mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa
Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amewahamasisha Waandishi wa Habari wa Tanzania
kushiriki vema katika kuwania tuzo za wanahabari wa Jumuiya za Mendeleo Kusini
mwa Bara la Africa (SADC).
Dkt. Abbasi ametoa rai kwa Waandishi wa Habari kushiriki tuzo
hizo jumatatu wiki hii wakati akiongea na waandishi wa Habari kuhusu hali ya
uchumi na utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyopo nchini.
“Tunawaomba wale wote ambao wanadhani wanavigezo basi
washiriki tuzo hizi za umahiri ambazo zinahusu waandishi wa habari za magazeti,
redio, televisheni na wapiga picha za habari”, alieleza Mkurugenzi wa Idara ya
Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Alieleza kuwa maelezo kamili juu ya tuzo hizo yanapatikana
katika tovuti ya Idara ya Habari ya www.maelezo.go.tz
hivyo wote wenye habari mahiri katika magazeti, vipindi vizuri vya luninga au
wapiga picha wahakikishe wanashiriki ili kushindana na waandishi wenzao kutoka
nchi za kusini mwa Afrika.
Mbali na tuzo za SADC, Dkt. Abbasi pia ameeleza kuwa tuzo
nyingine ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
inashindaniwa na Wanahabari na maelezo yake yanapatikana katika tovuti ya Idara
ya Habari.
Amewataka wanahabari kuandika habari zao kwa umahiri mkubwa
ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaweza kukidhi hata kupata tuzo za
waandishi bora kama hizo zilizojitokeza.
Pamoja na kuwataka waandishi wa habari kushiriki katika tuzo
hizo, pia amewataka waandihsi hao kuhakikisha wanapata vitambulisho vipya ya
Waandishi wa Habari (Press Cards) vya mwaka 2018 baada ya vile vya mwaka jana
kuisha muda wake.
“Kwa kweli mwaka huu tutakuwa wakali kidogo kwa wale ambao
hawatokuwa na vitambulisho hivi kwani mchakato wa kuvipata ni rahisi kwa sababu
tumeshawapa muda wa miaka mitano wa kwenda kusoma hivyo hatuhitaji vyeti,
kinachohitajika ni barua ya mwajiri au chombo cha habari unachofanyia kazi tu.”
Alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi amewakumbusha wanahabari ambao bado
kiwango chao cha elimu kipo chini ya kile kilichowekwa katika Sheria ya Huduma
za Habari namba 12 ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 kujiendeleza
kwani muda uliotolewa wa miaka mitano unaendelea unazidi kuisha.

0 Comments