Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatekeleza sera mbali mbali
zenye muelekeo wa kupunguza umasikini.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa Ufunguzi wa Soko jipya
la kisasa lililopo Konde, wilaya ya Micheweni, Pemba.
Makamu wa Rais alisema Sekta ya kilimo inatoa ajira kwa
zaidi ya asilimia 70 na inachangia kiasi cha asilimia 50 ya chakula kinacholiwa
Zanzibar, hivyo ni jukumu la Serikali kuweka mazingira bora kwa wananchi ili
waweze kujiletea maendeleo.
“Soko hili la kisasa
litapelekea kuongezeka kwa ajira, kupitia kuongezeka kwa shughuli za kibiashara
na kilimo, kuongezeka kwa uzalishaji, na uongezaji thamani wa mazao, hata
kuongezeka kipato cha mtu mmoja mmoja na
Taifa kwa ujumla”.
Makamu wa Rais alisema ni dhahiri kwamba kuondoka na
umasikini kutategemea sana mafanikio ya shughuli zinazotekelezwa katika sekta
ya kilimo “hivyo ni vyema tukaboresha kilimo kwa kubuni fursa zaidi na kuongeza
kipato kwa wananchi wetu”.
Makamu wa Rais alitoa wito kwa uongozi wa Shehia,
halmashauri, Wilaya na mkoa kuhakikisha kuwa soko linasimamiwa kwa ukaribu na
linatumiwa kwa kuzingatia taratibu zitakazohakikisha uendelevu wa huduma
zitakazotolewa na kuona malengo yaliokusudiwa yanafanikiwa ikiwamo kuwaletea
wananchi mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Mwisho Makamu wa Rais aliwataka wananchi kuendelea kuwa kitu
kimoja katika kulienzi soko ili liweze kuboresha maisha yao na ya vizazi
vijavyo
Wakati huo huo, Mhe. Hamad Rashid Mohamed - Waziri
wa Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi
Alisema kuwa maendeleo yanayojengwa leo ni mmoja
ya azma kubwa ya Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyesema
kuwa “Tunataka kuweka hali za wananchi
sawa” na ndio maana Rais Dkt. Ali Mohamed Shein amejitahidi kuleta
maendeleo sawa sawa kila pahala.

0 Comments