*Ni baada ya kuisababishia halmashauri hasara ya sh. milioni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi Bw. Alphonce Sebukoto na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.
Amechukua hatua hiyo baada Mwanasheria huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya sh. milioni 279.
Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Bw. Sebukoto leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ua Misungwi katika ukumbi wa Shule ya Msingi ya Mitindo Februari 19, 2018. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
“Mwanasheria
utasimama kazi kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo
husika na uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. Hatuta kuonea
lakini hatuwezi kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya.”
Amesema mwanasheria huyo Novemba 2017 wakati
alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi aliidhinisha malipo ya sh.milioni 279
zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Anthony
Bahebe.
Waziri Mkuu amesema Bw. Bahebe aliishtaki
halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi
wa maji Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim.
Amesema mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa
ukamilike 2015. Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari
hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu Desemba 2015.
“Mwanasheria amemlipa Mwenyekiti wa
Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri baada ya kuifikisha Halmashauri
yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati kazi yenyewe ilikuwa haijaisha na
aliharakisha malipo hayo kipindi ambacho Mkurugenzi hayupo.”
Waziri Mkuu amewakumbusha watumishi wa umma
kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa
majukumu yao. Amesema fedha alizolipwa Bw. Bahebe zingeweza kutumika katika
ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Awali, Waziri Mkuu alifungua
mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Mitindo iliyoko
wilayani Misungwi na kisha alikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 19, 2018.
0 Comments