WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya
Magu, Dkt. Nindwa Maduhu ahakikishe zahanati Bugabu inafunguliwa Februari 17,
2018.
Ametoa agizo hilo (Jumamosi, Februari 17, 2018) wakati akiongea
na watumishi na wananchi wa wilaya ya Magu katika kituo cha Afya cha Kahangara.
Alisema kama zahanati imekamilika na inavifaa vyote
vinavyotakiwa katika utoaji wa huduma kwa nini watumishi wasipelekwe ili
wananchi wahudumiwe.
Alitoa hilo baada ya wananchi kumuomba awasaidie kufunguliwa kwa
zahanati ya kijiji chao ili waweze kupata huduma za afya karibu na makazi yao.
Wananchi hao walidai kuwa kwa sasa wanalazimika kutembea umbali
wa kilomita tisa kufuata huduma za afya katika kituo cha Afya cha Kihangara.
Dkt. Maduhu alisema tayari watumishi walishahamishiwa katika
zahanati ya kijiji hicho na leo watakwenda na kuanza kuwahudumia wananchi.
Pia Waziri Mkuu amemtaka mganga huyo kuhakikisha dawa
zinazonunuliwa wilayani humo kulingana na magonjwa yanayopatikana ndani ya
maeneo yao.
Kabla ya kuzungumza na wananchi na watumishi, Waziri Mkuu
alikagua na kuweka jiwe la msingi la uboreshaji wa kituo cha Afya Kahangara.
Mradi wa kuboresha kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia watu
26,321 ulianza Oktoba 30, 2017 na umegharimu sh. milioni 50
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, FEBRUARI 18,
2018.

0 Comments