Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Waratibu wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) mahala pa kazi kutoka katika wizara mbalimbali nchini mjini Morogoro.
Baadhi ya Waratibu wanaosimamia masuala ya VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) katika taasisi za umma wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko (hayupo pichani) akifungua kikao kazi cha Waratibu hao mjini Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko akiwa katika picha ya pamoja na Waratibu wanaosimamia masuala ya VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) katika taasisi za umma mara baada ya kufungua kikao kazi cha Waratibu hao mjini Morogoro.
TAARIFA
KWA UMMA
Serikali imewataka Waratibu wanaosimamia masuala ya VVU, UKIMWI
na Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) katika taasisi za umma kutekeleza wajibu wao
ili kupata takwimu sahihi za watumishi wanaoishi na VVU, UKIMWI na wenye
Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa mpango wa kupambana na magonjwa
hayo yanayoathiri utendaji kazi wa
watumishi kwa kiasi kikubwa.
Wito huo umetolewa leo mjini Morogoro na Naibu Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy
Mwaluko wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Waratibu wa VVU, UKIMWI
na Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) mahala pa kazi kutoka katika wizara
mbalimbali nchini.
Bi. Mwaluko amesema, kukosekana kwa taarifa sahihi za watumishi
wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI, kumekwamisha mpango thabiti wa
Serikali wa kukabiliana na changamoto ya maambukizi mapya kwa Watumishi wa Umma
nchini.
Aidha, Bi. Mwaluko amehoji uhalisia wa takwimu zilizopo sasa za watumishi
wa umma 1852 waliobainika kuishi na VVU/UKIMWI iwapo zinatoa taswira halisi ya
tatizo lililopo.
Bi. Mwaluko ametoa angalizo kwa waratibu kusimamia vizuri suala
la afya za watumishi kwani lina athari kubwa kiutendaji lisiposimamiwa vema.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Anuai za Jamii Ofisi ya
Rais-Utumishi, Bi. Leila Mavika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Tendaji
ya Kitaifa inayosimamia utekelezaji wa shughuli za VVU,
UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa (MSY) mahala pa
kazi, amesema kuna mwitikio hafifu wa watumishi wa umma kupima afya zao kwa
sababu ya hofu ya kunyanyapaliwa, hivyo amewataka waratibu kuweka mkakati
madhubuti utakaowawezesha watumishi hao kuwa huru kujitokeza na kupima afya.
Naye, Katibu wa Kamati Tendaji ya Kitaifa ambaye pia ni
Afisa Mwitikio wa taasisi za Umma kutoka TACAIDS, Dkt. Ameir Hafidh,
amesema kuwa Serikali imeweka mkakati wa
kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 asilimia tisini ya wanaoishi na VVU/UKIMWI
watakuwa wametambua hali zao na kuanza kutumia dawa za kupunguza makali kwa
usahihi.
0 Comments