Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Anuai
za Jamii, Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika akisisitiza
jambo katika kikao kazi cha Kamati Tendaji ya Kitaifa
inayosimamia utekelezaji wa shughuli za VVU, UKIMWI na
Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa (MSY) mahala pa kazi mjini Morogoro.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Tendaji ya Kitaifa inayosimamia utekelezaji wa shughuli
za VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa (MSY)
mahala pa kazi wakiwa katika kikao kazi mjini Morogoro.
AFYA
ZA WATUMISHI ZIZINGATIWE ILI KUBORESHA UTENDAJI
Waajiri nchini
wameelekezwa kuzingatia afya bora za watumishi katika taasisi zao kwani
watumishi ndio nguvu kazi ambayo inawezesha shughuli kufanyika kwa
ufasaha na kuleta tija kwa maendeleo ya taifa.
Hayo yamebainishwa na Kaimu
Mkurugenzi wa Kitengo cha Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Kamati Tendaji ya Kitaifa inayosimamia utekelezaji wa shughuli
za VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa (MSY)
mahala pa kazi wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo mjini Morogoro.
Bi. Mavika amesema
kuwa, kikao kazi hicho kimelenga kubadilishana taarifa, kutathmini hali
halisi ya utekelezaji wa AFUA za UKIMWI mahala pa kazi,
pamoja na kubuni mikakati itakayowezesha Taasisi za Umma kutekeleza kisheria
mwongozo na waraka unaohusu utoaji wa huduma kwa watumishi wanaoishi na VVU na UKIMWI mahala
pa kazi.
Bi. Mavika ameongeza
kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Rais-Utumishi, imetoa miongozo mbalimbali
ikiwemo Mwongozo wa Kudhibi VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa mahala
pa kazi katika Utumishi wa Umma wa mwaka 2014 unaoelekeza utaratibu na usimamizi wa
masuala ya UKIMWI mahala pa kazi.
Aidha, Bi. Leila
amesema, Serikali imetoa Waraka wa Utumishi Na. 2 wa mwaka 2014 kuhusu Kudhibiti
Virusi vya UKIMWI, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa mahala pa kazi
katika Utumishi wa Umma, waraka huo unawaelekeza waajiri namna ya kutoa
huduma kwa watumishi wanaoishi na Virusi vya UKIMWI na UKIMWI.
Kwa Upande wake,
Katibu wa Kamati hiyo Tendaji ya Kitaifa ambaye pia ni Afisa Mwitikio wa
taasisi za Umma kutoka TACAIDS, Dkt. Ameir Hafidh amesema kuwa, jukumu
lake kubwa ni kuhakikisha suala la UKIMWI sehemu za kazi katika sekta
ya Umma linazingatiwa kwa mujibu wa Mwongozo na Waraka husika.
Dkt. Hafidh
amesisitiza kuwa ni jukumu la mwajiri kuhakikisha anampatia huduma stahiki
mtumishi anayeishi na Virusi vya UKIMWI na UKIMWI mara baada ya kujiweka wazi
kwa mwajiri.
Wajumbe wa Kamati Tendaji
Kitaifa wanaoshiriki katika kikao hicho ni kutoka Ofisi ya Rais-Utumishi, Tume
ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Chuo
cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Tume ya Utumishi wa Umma Tanzania na
Taasisi ya Chakula na Lishe.
IMETOLEWA
NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 10 MEI, 2018
0 Comments