Subscribe Us

header ads

Watoto Tisa Wenye Matatizo ya Moyo Kwenda Kutibiwa Nchini Israel

Watoto tisa wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wanaondoka leo tarehe 28/5/2018 kwenda nchini Israel kwa ajili ya matibabu ya moyo. Katika safari yao ya matibabu nchini humo watoto wataambata na  wauguzi pamoja na wazazi wao.

Safari hiyo ya matibabu nchini Israel inahusisha watoto wenye umri wa miezi tisa  hadi miaka 14 imeratibiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya  Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s  Heart – SACH) ya nchini humo. 
  
Taasisi yetu inatibu magonjwa mengi ya moyo (kwa asilimia 90) kwa watoto  kupitia  wataalamu wazalendo tulionao. Hata hivyo tunamkataba na Israel kwa baadhi ya wagonjwa wachache ambao ni asilimia 10 wanaohitaji utaalamu wa hali ya juu zaidi kuliko uliopo hapa nchini kwa sasa.

Tunaushirikiano mzuri na nchi ya Israel kwani gharama za matibabu ya watoto hawa zinagharamiwa na SACH. Aidha tuna madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo sita   na wauguzi wanne ambao wamesoma nchini Israel na hivi sasa wanatibu wagonjwa katika Taasisi yetu. Daktari wetu mmoja na wauguzi wawili bado wanaendelea na masomo nchini humo hii itasaidia kwa siku za mbeleni zaidi ya asalimia 95 ya watoto watatibiwa  hapa nchini.

Hili ni kundi la sita   la watoto kwenda kutibiwa magonjwa ya moyo nchini Israel tangu mwaka 2015 ambapo Taasisi ya Moyo ilianza ushirikiano  na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart –SACH)  wa kuwapeleka wagonjwa nchini humo. Hadi sasa watoto 56 wameshatibiwa nchini humo na wanaendelea vizuri.

Taasisi inaendelea kutoa wito kwa wazazi na walezi wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni. Mtoto akianza kuuguwa magonjwa ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha mtoto Hospitali na kufanyiwa vipimo  ndipo inagundulikwa kuwa mtoto anasumbuliwa na magonjwa ya moyo.

Kwa wamama wajawazito wafanye uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni anamatatizo ya moyo au la. Kupitia kipimo hiki  mtoto akigundulika kuwa  na tatizo la moyo ataweza kupatiwa  matibabu kwa wakati  na hivyo kuwa na afya njema kama watoto wengine.

Imetolewa na :

Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete

28/05/2018

Post a Comment

0 Comments