....................................................................................................................
Na
Happiness Shayo - Rwanda
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda
imekubaliana kuwaunganisha wafanyabiashara wa Sekta ya Utalii wa nchi hizo ili
kukuza utalii.
Hayo
yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)
katika Maadhimisho ya Wiki ya Utalii ya Rwanda yanayoendelea nchini humo.
“Kikubwa
tumeweza kukutana na Rais wa wafanyabiashara za kitalii wa hapa nchini
Rwanda na tumeomba wafanyabiashara wa huku kushirikiana na wa kwetu kukuza
Sekta ya Utalii” amesema Mhe. Masanja.
Aidha,
Mhe. Masanja amewataka Watanzania kuwa wazalendo kwa kutangaza vivutio vya
utalii vilivyoko nchini mwao.
“
Nawaomba Watanzania kwa umoja wetu tuendelee kuwa wazalendo, tuipende
nchi yetu na tuendelee kuitangaza nchi yetu kama ambavyo wenzetu wa Rwanda
wanavyofanya” Mhe. Masanja amesisitiza.
Naye,
Naibu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Zephanie Niyonkuru amesema
kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Utalii ya Rwanda yamelenga katika kuibua ubunifu
katika Sekta ya Utalii nchini humo na kutoa tuzo kwa mshindi.
Ameongeza
kuwa pia maonesho hayo yanatoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na wa
Kimataifa kuuza bidhaa na huduma zao kwa wadau wengi kutoka Bara la Afrika.
Kwa
upande wake Afisa Masoko Mkuu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania, Bernard
Mtatiro amesema kupitia Wiki ya Utalii ya Rwanda Tanzania itapata fursa ya
kutangaza mazao mapya ya utalii kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tumejipanga
kutangaza mazao mapya ya utalii kwa mfano Utalii wa Mchezo wa gofu, reli ya
mwendokasi (SGR), Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere na Hifadhi ya Taifa ya
Nyerere” amefafanua Bw. Mtatiro.
Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya “Kujenga Upya Utalii kwa Ukuaji Endelevu”yamehudhuriwa na washiriki kutoka nchi za Tanzania, Ghana, Botswana Kenya, Nigeria, Kongo, Afika Kusini, Somalia, Zimbwabwe pamoja na wadau wa utalii kutoka Dubai.
No comments:
Post a Comment