Subscribe Us

header ads

BAKWATA Singida Kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki ili kujikwamua kiuchumi

Masheikh wa Wilaya  na Makatibu, na Masheikh wa Kata wakimsikiliza Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro Issa ( hayupo pichani ) namna ya kuanzisha na kuendesha miradi ya maendeleo.
 Mratibu wa Taifa wa BAKWATA Online Academy, Maadhi Abdulkarim akizungumzi miradi ya maendeleo wakati wa kikao hicho.
Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro Issa akizungumza wakati wa kikao cha mpango kazi kilichofanyika msikiti mkuu wa Taqwa Manispaa ya Singida.
......................

Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA

BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida,limepanga kuanzisha miradi ya maendeleo ukiwamo wa ufugaji nyuki kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi wa kila kitu kutoka kwa wafadhili.

Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro Issa, alisema hayo tarehe 21- 1- 2023 wakati wa kikao cha mpango kazi kilichofanyika msikiti mkuu wa Taqwa Manispaa ya Singida ambacho kiliwashirikisha masheikh wa wilaya, Wenyeviti wa BAKWATA wilaya na makatibu na kata.

Sheikh Issa alisema katika mradi wa nyuki, wamekubaliana kila kata itachangia Sh.80,000 kwa ajili ya kununua mizinga ya nyuki 100 ambayo itawekwa eneo lenye ekari 464 lililopo kata ya Misughaa wilaya ya Ikungi.

"Tumekubaliana tuanze na mradi huu wa nyuki kwasababu unatoa tija haraka kwani ndani ya miezi sita tunaanza kuvuna asali na kimsingi mradi huu utawasaidia viongozi kupata kipato na kuendesha ofisi pasi kutegemea wafadhili," alisema.

Alisema waislamu wote mkoani Singida wajitokeza kuunga mkono miradi ambayo imepangwa kuanzishwa na BAKWATA ukiwamo umaliziaji wa ujenzi wa hospitali iliyopo wilayani Iramba ambayo ilitolewa na mdau mmoja kwa baraza hilo.

Aidha, Sheikh Issa alisisitiza suala la nidhamu kwa viongozi lizingatiwe na waumini wote kwani jambo hilo limesisitizwa hata kwenye katiba ya Bakwata.

Naye Mratibu wa Taifa wa BAKWATA Online Academy, Maadhi Abdulkarim, alisema kubuni miradi ya maendeleo kutaliwezesha baraza hilo kusonga mbele kiuchumi na kuufanya Mkoa wa Singida kubwa mkoa wa mfano nchini.

Abdulkarim ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mufti (Mufti Development Fund), alisema heshima ya muumini ni kuwa na kazi inayomuingizia kipato kwani bila hivyo hawezi kuheshimika na jamii.

"Uchumi unamuongezea mtu dhwawabu na heshima kwani umaskini sio sifa na kiongozi mzuri ni lazima awe 'smart' zaidi kifikira na kiutendaji," alisema.

Aliongeza kuwa viongozi na waumini kwa ujumla lazima wafahamu kuwa nadharia ya kazi za uongozi ni kupanga,kuratibu,kuongoza na kudhibiti.

Naye Mwenyekiti wa BAKWATA Wilaya ya Singida vijijini, Issa Juma Mwiru, alisema mafunzo waliyopewa yatawafanya kubadilika kiutendaji na kubuni miradi ya maendeleo ambayo itawaingizia kipato.

Post a Comment

0 Comments