Dar
es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kesho tarehe 05 Juni, 2023 ameialika
timu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) kwa chakula cha jioni Ikulu,
Jijini Dar es Salaam kwa lengo kuipongeza kwa kufanya vizuri katika michuano ya
soka ya kugombea Kombe la Shirikisho Barani Afrika iliyohitishwa jana Jijini
Algers, Algeria.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson
Msigwa amesema Rais Samia amewapongeza Yanga kwa kucheza vizuri katika mchezo
wa pili wa fainali hapo jana kwa kuwafunga wenyeji wa mchezo huo bao 1-0 na
hivyo kuwa na matokeo ya jumla ya mabao 2-2 japokuwa hawakufanikiwa kutwaa
ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kutokana na kuruhusu kufungwa
mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza wa fainali uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin
Mkapa Jijini Dar es Salaam Tarehe 28 Mei, 2023.
Msigwa amebainisha kuwa pamoja na
kutotwaa ubingwa, Mhe. Rais Samia anatambua kuwa Yanga wameipa heshima kubwa
Tanzania na anawapongeza Wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo
ambao ni Mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
Timu ya Yanga, viongozi na mashabiki wanatarajiwa kurejea hapa nchini baadaye leo kwa ndege iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono timu hiyo iliyokuwa ikiiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kimataifa.
0 Comments