Majadiliano yakifanyika wakati wa ziara hiyo mkoani Mtwara ya kufanya tathmini katika kata za Madimba na Msimbati ili kuona hali halisi kabla ya kuanza utekelezaji.
...................................................
Na Veronica Simba, Mtwara
WAKALA wa Nishaji Vijijini (REA) umeanza
utekelezaji wa maagizo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa
kuwafikishia huduma ya umeme wakazi wa Madimba na Msimbati kwa kufanya tathmini
katika maeneo hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi
Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu alifanya ziara ya kufanya tathimini katika
kata za Madimba na Msimbati ili kuona hali halisi kabla ya kuanza utekelezaji.
Naibu Waziri Mkuu, Dkt Doto Biteko, akiwa katika
ziara ya kazi mkoani Mtwara hivi karibuni aliitaka REA kuangalia ni namna gani
inaweza kuwaunganishia umeme wananchi wa maeneo hayo na kujenga miundombinu ili
waweze kunufaika na nishati ya gesi asilia inayozalishwa katika eneo hilo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na Madiwani wa
Kata za Msimbati na Madimba, Balozi Meja Jenerali Kingu amesema REA
itahakikisha maelekezo hayo yanatekelezwa ambapo Novemba 18, 2023 watakutana na
mkandarasi kwa ajili ya kujadili ujenzi wa miundombinu ya umeme katika kata
hizo.
“Tutahakikisha utekelezaji wa haraka unafanyika
na wataalamu wanapita ili kuona hali halisi na uhitaji katika maeneo husika”
Aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuwapatia
ushirikiano wataalamu wa REA na mkandarasi ili kuharakisha uratibu wa kazi
hiyo.
Aidha, alisema Bodi na Menejimenti ya REA
watafuatilia kwa karibu utekelezaji wa agizo la Naibu Waziri Mkuu la
kuyafikishia maeneo hayo umeme.
Alitaka taarifa zitolewe haraka endapo kutakuwa
na changamoto katika utekelezaji wa mradi huo ili zipatiwe ufumbuzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati Vijijini,
Mhandisi Jones Olotu aliwahakikishia Maafisa Watendaji wa Kata hizo mbili kuwa
wiki ijayo wakandarasi watafika kukutana nao kwa ajili ya kuoneshwa maeneo na
vijiji vinavyotakiwa kufikishiwa umeme.
Diwani wa Kata ya Msimbati, Rashid Linkon
aliishukuru serikali kwa uamuzi wake wa kuhakikisha wanapata umeme na kunufaika
na rasilimali ya gesi asilia inayopatikana eneo hilo.
Alisema upatikanaji huo wa umeme utaleta hamasa
kwa wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya uzalishaji wa gesi.
No comments:
Post a Comment