Thursday 19 October 2023

RAIS. DKT SAMIA: MKOA WOTE WA SINGIDA KUPATA UMEME IFIKAPO JUNI 2024

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Iramba Kata ya Shelui Oktoba 18, 2023 kwenye hafla ya uzinduzi wa kuwasha umeme katika vijiji 131 kupitia mradi wa R3R2  mkoani Singida ambao umetekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Rais Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili viwanja vya Shule ya Msongi ya Shelui kwa ajili ya kuongoza uzinduzi huo. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya REA Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu na katikati ni Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijiji (REA) Mhandisi Hassan Saidy akijitambulisha wakati wa uzinduzi huo.
Uzinduzi ukiendelea.
Taswira ya uzinduzi huo.
...................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema Mkoa wa Singida hadi ifikapo Mwezi Juni mwaka 2024 utakuwa umepata umeme maeneo yote.

Hayo aliyasema Oktoba 18, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Iramba Kata ya Shelui kwenye hafla ya uzinduzi wa kuwasha umeme katika vijiji 131 kupitia mradi wa R3R2  mkoani Singida ambao umetekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“Wilaya ya Iramba ni sehemu ya Mkoa wa Singida ni sehemu ya mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya 3 Mzunguko wa Pili ambao unalenga kuvifikia vijiji 178 katika Wilaya ya Singida, Singida Vijijini, Ikungi, Manyoni, Mkalama na Iramba,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alisema asilimia 90 ya kazi yote imekwisha kamilika na kuwa Juni 2024 mwakani Singida yote kama mkoa itakuwa inawaka umeme na akatumia nafasi hiyo kuwapongeza sana wana Singida.

Alisema kukamilika kwa kazi hiyo itakuwa ndani ya muda waliowekewa na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kupeleka umeme nchini kote ifikapo 2025 na kwa Mkoa wa Singida kabla ya muda huo utakuwa umewashwa umeme.

Rais Samia alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua za muda mfupi na mrefu za kuimarisha gridi ya Taifa ili kuondokana na changamoto ya umeme kukatika mara kwa mara na kuwa kufikisha umeme ni jambo moja na kupatikana kwa umeme wa uhakika ni suala jingine.

Aidha, Rais Samia alisema  Serikali ipo makini katika kutekeleza ahadi zote walizozitoa wakati wakiomba dhamana ya kuliongoza taifa kupitia CCM.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijiji (REA) Mhandisi Hassan Saidy akisoma hotuba yake mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo alisema  Mradi wa R3R2 una tekelezwa katika vijiji 4071 kwa gharama ya Sh.Trilioni 1.6 na utakamilika Juni 2024 na kufanya vijiji vyote 12,318 kuwa na umeme.

Alisema mpaka sasa vijiji 11,000 vina umeme, 1300 vilivyobaki vitafikiwa na umeme ifikapo juni 2024 na kuwa Mkoa wa Singida una jumla ya vijiji 441 ambapo mpaka sasa vijiji 397 vina umeme, vijiji 44 vilivyobaki wakandarasi wapo kazini na vitapata umeme mpaka Desemba 2023.

Mhandisi Saidy alisema Mkoa wa Singida una jumla ya miradi 4 inayopeleka umeme kwenye vijiji, vitongoji, mitaa, migodi, pampu za maji, vituo vya afya, maeneo yq biashara na kilimo kwa jumla ya takribani Sh. Bilioni 86.

No comments:

Post a Comment