Baadhi
ya wakazi wa Iramba waliojitokeza siku ya siku ya kwanza ya huduma tembezi za
kibingwa.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe akihutubiwa wakati wa uzinduzi
rasmi wa huduma tembezi za madaktari bingwa Mkoani Singida.
Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Singida John Mwombeki akisoma taarifa ya hali ya afya Mkoa wa
Singida wakati wa uzinduzi wa huduma tembezi za kibingwa.
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Macho akimhudumia mteja siku ya kwanza ya huduma tembezi
za kibingwa.
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Meno akimhudumia mteja siku ya kwanza ya huduma tembezi
za kibingwa.
.................................................................................................
Na Mwandishi Wetu Iramba
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amezindua rasmi huduma tembezi
za madaktari bingwa Mkoani Singida, na kuwasihi wananchi Mkoani Singida
kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo za kibingwa.
Huduma
hizo za kibingwa zilizozinduliwa Wilayani Iramba katika hospitali ya Kiomboi
zitahusisha huduma za kibingwa za upasuaji, meno, macho, upasuaji wa mifupa,
huduma za kibingwa za magonjwa ya watoto, wanawake na huduma za kibingwa za
mionzi.
Mhandisi
Mtigumwe amesema matarajio ya Mkoa ni kuwa huduma tembezi za kibingwa
zitasaidia kutambua na kutibu magonjwa mbalimbali kabla hayajafikia hatua ya
usugu na kupunguza gharama za rufaa za wagonjwa kwenda nje ya mkoa.
'Huduma
tembezi za kibingwa zitawasaidia wananchi kutambua uwepo wa huduma za kibingwa
katika mkoa wa singida na kupata matibabu kwa gharama nafuu' amengeza Mhandisi
Mtigumwe.
Naye
Mganga Mkuu wa Mkoa Dokta John Mwombeki akisoma taarifa ya hali ya afya Mkoa wa
Singida amesema wazo la kuanzisha huduma tembezi za kibingwa limetokana na idadi
kubwa ya operesheni zilizofanyika kwa mwaka 2015/2016 na pia mkutano wa wadau
wa afya mkoani hapa kuafiki wazo la kuanzisha huduma hiyo.
"Kwa
kipindi cha mwaka 2015/2016 jumla ya operesheni kubwa na ndogo 4,836
zimefanyika katika hospitali mbalimbali mkoani hapa, aidha Idara ya macho
katika hospitali ya Mkoa imefanya jumla ya operesheni kubwa na ndogo
2,020" ameongeza Dokta Mwombeki.
Dokta
Mwombeki amesema uwepo wa madaktari bingwa 11 mkoani Singida pia umekuwa chachu
ya utekelezaji wa huduma hiyo huku Mkoa ukifanya jitihada za kuazima madaktari
wengine katika mikoa jirani ya Dodoma na Manyara.
Baadhi
ya wagonjwa waliohudhuria katika siku ya kwanza ya zoezi hilo huku huduma hiyo
ikitarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tano wilayani hapo wameeleza shauku na
furaha yao ya kusogezewa huduma za kibingwa katika halmashauri zao.
"Nilikuwa
naumwa jino ambalo limeota vibaya, niliambiwa nitaweza kufanyiwa operesheni
katika hospitali kubwa kama Muhimbili lakini hawa madaktari wametusaidia ,
nimepata huduma haraka na kwa gharama nafuu, nawasihi wenzangu waje kwa
wingi" amesema Bi Neema Josseph Mkazi wa Kijiji cha Kizaga Wilayani
Iramba.
Naye
Mzazi wa mtoto Jonas Masaka amesema huduma za kibingwa zitamsaidia mtoto wake
mwenye matatizo ya macho na hiyo kumpunguzia gharama ya kumpeleke katika
hospitali kubwa kutibu tatizo la macho linalomsababisha mtoto huyo kushindwa
kusoma vizuri.
Huduma
ya tembezi za kibingwa Mkoani Singida zitafanyika katika Wilaya zote tano za
Mkoa nwa Singida na hvyo kupunguza wagonjwa wa rufaa watakaopelekwa hospitali
za Bugando, KCMC na Muhimbili.




