Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Waziri
wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi
Ally Karume mara baada ya kumtembelea ofisini kwake Kisiwani Unguja.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akijadiliana jambo na
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Balozi Ally (kulia) Karume wakati alipotembelea taasisi zilizochini ya Wizara
hiyo. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hiyo Mustafa Abood Jumbe.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), akipata
maelezo ya kiutendaji kutoka kwa Meneja wa Mamlaka wa Usafiri wa Anga Tanzania
(TCAA) upande wa Zanzibar, Mbarouk Hamis Hamad wakati alipokagua utendaji wa
taasisi hiyo.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa wakati
viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Kisiwani Unguja. Kulia ni
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Balozi Ally Karume.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mustapha Abood Jumbe afafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati)
katika kikao kazi mjini Unguja.
............................................................................................
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali iko katika
hatua za mwisho za kutangaza zabuni kwa ajili ya ununuzi wa rada sita za kisasa
kwa ajili ya kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa safari za anga hapa nchini.
Prof. Mbarawa
amesema hayo mjini Unguja mara baada ya kukagua shughuli zinazofanywa na
Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na Uwanja wa
Ndege wa Zanzibar ambapo amesisitiza umuhimu wa kufata sheria katika kumpata
mzabuni.
“Tumejipanga
kuhakikisha kwamba miundombinu ya safari za anga nchini inaimarika ili kuvutia
utalii na usalama wa abiria wa usafiri wa anga”, amesema Prof. Mbarawa.
Ameitaka TCAA
kuhakikisha kwamba marubani wanaopewa vibali vya kurusha ndege nchini wanakidhi
vigezo vya kimataifa ili kuufanya usafiri wa anga kuwa salama na wa uhakika.
Naye Waziri wa
Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi
Ally Karume amempongeza Prof. Mbarawa kwa ushirikiano anaoufanya kati ya Wizara
hizo na kusisitiza kuwa hali hiyo itaongeza ufanisi katika usimamizi wa
shughuli za Serikali na kuleta tija kwa wananchi.
“Huduma wanazozipata
bara ni vyema na sisi Zanzibar tukanufaika nazo ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya
Muungano ili kuleta usawa kwa wananchi wa pande zote za Muungano”, amesisitiza
Balozi Karume.
Katika hatua
nyingine Profesa Mbarawa amezungumzia umuhimu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kubadilisha mfumo wa masafa wa 700MHZ kutoka kwenye analogia kwenda Digitali
ili kuuwiana na upande wa Tanzania Bara na hivyo kuondoa muingiliano wa
mawasiliano.
Profesa Mbarawa yupo
Mjini Unguja katika ziara ya kukagua taasisi zilizo chini ya wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano na kubadilishana uzoefu na viongozi wa wizara hiyo
(Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji) kwa upande wa Zanzibar.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano




