Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), limepokea kwa masikitiko taarifa za kupata ajali kwa
msafara wa timu ya Ruvu Shooting FC iliyotokea leo barabara ya Manyoni
mkoani Singida wakati kikosi hicho kikitokea Shinyanga kwenda Pwani.
Taarifa kutoka Singida zinasema
gari hilo lilipata ajali baada ya kupasuka tairi moja la mbele hivyo
kuyumba na kuacha njia eneo la Itigi – kilometa 200 kutoka Singida
mjini kuelekea Manyoni hivyo kutoka barabarani kuu kabla ya kugonga
mti.
Taarifa hizo zilizothibitishwa na
Masau Bwire, zinasema wachezaji watatu akiwamo Bwire mwenyewe ndio
waliopata majeraha na kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Singida kwenda
kutibiwa. Wachezaji hao ni Yussuf Nguya, Abdul Mpambika na Saidi
Dilunga.
Timu hiyo ilikuwa mkoani
Shinyanga ilipocheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa
2016/17 dhidi ya Stand United na kupoteza kwa mabao 2-1, hata hivyo
imebaki kucheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu ujao baada ya kushika nafasi
ya saba.
Mara baada ya kupata taarifa
hizo, Rais wa TFF Jamal Malinzi mara moja ametuma salamu za kuwapa pole
uongozi wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania pamoja na
timu nzima ya Ruvu Shooting.
“Nawapa pole viongozi wote,
makocha na wachezaji. Na kwa wachezaji ambao wamejeruhiwa na viongozi
wote waliojeruhiwa akiwamo ndugu yetu Masau Bwire, nawaombea kwa
Mwenyezi Mungu wapone haraka,” amesema Malinzi.
Rais Malinzi alimshukuru Mungu
kwa kuepusha vifo kwa wanafamilia hao wa mpira wa miguu hasa wakati huu
Watanzania wakiwa makini kufuatilia maendeleo ya timu za taifa.
Taifa Stars – timu ya taifa ya
wakubwa inajiandaa kwenda kambini Misri kujiandaa kucheza na Lesotho
hapo Juni 10, 2017; Timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ na Serengeti
Boys – timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ambayo
kwa sasa inapambana kuwania Kombe la Afrika katika fainali zinazofanyika
Gabon.

0 Comments