Frank
Mvungi-Maelezo
Katika Kuhamasisha Ujenzi
wa Uchumi wa Viwanda, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) limeanzisha
Mkakati wa Wilaya Moja Bidhaa Moja (ODOP) ili kuchochea maendeleo ya Viwanda
vidogo kwa lengo la kuongeza kipato na ajira kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa
maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, Afisa Mwandamizi Uendelezaji
Biashara wa SIDO Bw. Stephen Bondo amesema dhamira ya Shirika hilo ni
kuhakikisha kuwa kuna viwanda katika Halmashuri zote kwa kufuata mpango wa
Wilaya moja Bidhaa moja.
“Mkakati huu unakusudia
kuibua na kuendeleza bidhaa moja kwa awamu katika Wilaya kwa kuzingatia
rasilimali zilizopo katika Wilaya husika kwa kuhakikisha kuwa wadau wanachagua
na kuwekeza katika viwanda vidogo na kuzalisha bidhaa ili kuweza kuharakisha
maendeleo ya kiuchumi Vijiji,” alisisitiza Bondo.
Bondo lifafanua kwa kusema
kuwa nchi ya Japan imefanikiwa katika sekta ya viwanda kwa kutumia mfumo huo
ambao umeteklezwa katika Taifa hilo hadi ngazi ya Vijiji na kuchochea maendeleo
yanayoonekana leo hii katika Taifa hilo.
Akizungumzia malengo ya
ODOP, Bondo amesema kuwa ni pamoja na kutumia rasilimali au malighafi, utaalamu
na ujuzi unaopatikana katika Wilaya husika na kuwawezesha wale wanaotaka
kuanzisha viwanda kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa katika Wilaya husika
hadi kufikia kuwa bidhaa.
Aliongeza kuwa eneo
jingine la utekelzaji wa mpango huo ni kujenga uwezo kwa wajasiriamali vijijini
katika mbinu za kibiashara na teknolojia ili kuweza kushindana katika soko la
Wilaya, Mkoa, Taifa na Kimataifa.
Pia kujenga mahusiano ya
Viwanda vidogo na vikubwa kwa viwanda vikubwa kuwa na mikataba ya kuboresha na
kutumia bidhaa za viwanda vidogo ili kupanua soko la viwanda vidogo.
Kwa upande wake Meneja
Masoko wa SIDO Bi. Lilian Masawe amesema wanachi wajitokeze katika Wilaya zao
kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuanzisha viwanda katika maeneo yao kwa
kuwa malighafi zipo na SIDO iko tayari kusaidia.
Alitaja baadhi ya Wilaya
zilizofanikiwa kutekeleza mpango huo kwa kushirikiana na wadau kuwa ni Geita,
Longido,Monduli,Singida na Wilaya zote hapa nchini kwa kuwa mpango huo
unatekelezwa katika Mikoa yote, dhamira ikiwa ni kujenga Tanzania ya viwanda
kuanzia ngazi ya Wilaya,Vijiji , Mikoa na Taifa.

0 Comments