Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nsele kilichopo kata ya Kilondo wilayani Ludewa mkoani Njombe katika ziara yake ya kukagua huduma za mawasiliano na maeneo ya kujenga bandari kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa aliyoifanya kuanzia kata ya Manda iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe hadi Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya.
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imetenga shilingi milioni 358 kwa ajili ya kulipa fidia
nyumba na ardhi za wananchi waishio mwambao wa Ziwa Tanganyika kwa ajili ya
kupisha upanuzi na ujenzi wa bandari za Ziwa hilo
Hayo yameelezwa na
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake aliyoifanya ya
kukagua bandari za Ziwa Nyasa kuanzia bandari ya Manda iliyopo wilaya ya Ludewa
mkoani Njombe hadi bandari ya Itungi iliyopo wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya.
Katik ziara hiyo, Meneja
wa Mamlaka ya Bandari za Ziwa Nyasa Bwana Ajuaye Heri Msese amesema kuwa
Mamlaka ya Bandari Tanzania imetenga fedha hizo kwa ajili ya kulipa fidia
wananchi wa maeneo ya mwambao wa Ziwa Nyasa waliojitolea maeneo yao ili kupisha
upanuzi na ujenzi wa bandari zilizopo ndani ya Ziwa Nyasa kuanzia bandari ya
Lipingu iliyopo Wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe hadi bandari ya Matema iiyopo
wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.
Naye Mkuu wa Wilaya wa
Ludewa Bwana Andrea Tsere amemueleza Mhandisi Nditiye kuwa tayari wamekamilisha
kazi ya kuhakiki malipo ya fidia za wananchi waliotoa ardhi zao eneo la Manda
na Lupingu. “Wanachi wa eneo la Manda watalipwa shilingi milioni 192 ambapo
wametoa eneo la ukubwa wa hekari 24 na wa Lupingu wametoa eneo ukubwa wa hekari
10.6 na watafidiwa shilingi milioni 166, amesema Tsere”.
Bwana Msese amesema
kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania inakamilisha ujenzi wa meli ya mizigo na
abiria na itaanza kazi ya kusafirisha abiria na mizigo ndani bandari za Ziwa
Nyasa mwezi Agosti mwaka huu ambapo meli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria
mia mbili na mizigo tani mia mbili kwenye jumla ya bandari kumi na tano
zilizopo ndani ya mwambao wa ziwa Nyasa.
Naye Mbunge wa Jimbo
la Ludewa Mhe. Deo Ngalawa amemshukuru Mhe. Mhandisi Nditiye kwa niaba ya
wananchi wake kwa kufika kwenye makazi ya wananchi hao waishio kwenye mwambao
wa Ziwa Nyasa na kukagua mahitaji ya usafiri wa majini wa abiria na mizigo wa
Ziwa hilo ambapo Serikali tayari imetenga fedha kulipa fidia wananchi waliotoa
maeneo yao kupisha ujenzi na upanuzi wa bandari za Ziwa hilo.
Ujenzi wa bandari hizo
na utoaji wa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo ni ukamilishaji wa ahadi
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa
wananchi waishio kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa ambao wanategema Ziwa hio kwa
kiasi kikubwa kwa shughuli za kiuchumi, biashara na kijamii ambazo zitachangia
ukuaji wa uchumi wa wananchi hao na taifa kwa ujumla.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilano
0 Comments