TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania anaondoka nchini Aprili 15,
2018 kwenda London, Uingereza kushiriki
kwenye Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaotarajiwa
kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 20 Aprili, mwaka huu akimwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mkutano huo ambao Kaulimbiu yake ni “Kuelekea Mustakabali wa Pamoja” utafanyika
chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa Theresa May na utafunguliwa
na Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza.
Majadiliano ya Mkutano wa CHOGM 2018 yatajikita kwenye maeneo manne
makuu ya kipaumbele ambayo yatajadili namna Jumuiya ya Madola inaweza kufikia mustakabali
wenye ustawi zaidi; mustakabali endelevu zaidi; mustakabali wenye haki zaidi;
na mustakabali wenye usawa zaidi.
Mijadala katika maeneo hayo ya kipaumbele itahusisha masuala mbalimbali
ikiwemo, kukuza zaidi biashara na uwekezaji baina ya nchi za Jumuiya ya Madola
kwa manufaa ya nchi wanachama na Jumuiya nzima; kukuza na kuendeleza misingi ya
demokrasia; ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo endelevu pamoja na
masuala ya uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uhalifu wa kimtandao na
usafirishaji wa binadamu.
Jumuiya ya Madola ilianzishwa mwaka 1949 kupitia Tamko la London ambalo lilikuwa
ni matokeo ya Mkutano wa Mawaziri Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola. Jumuiya ya Madola ina wanachama 53 ambapo kati
ya hizo, nchi 19 ni za Afrika, 7 ni kutoka Asia, 13 ni kutoka nchi za Carribean
na Mabara ya Amerika, 11 ni kutoka eneo la Pacific na nchi 3 ni kutoka Ulaya.
Ujumbe wa Makamu wa Rais unajumuisha Mheshimiwa Dkt. Balozi Augustine
Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja
na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa
Afrika Mashariki.
Makamu wa Rais na ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Aprili 22, mwaka
huu.
Imetolewa na:
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
15/4/2018

0 Comments