Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.
Serikali imeeleza kuwa inalinda
thamani ya Shilingi kwa kudhibiti mfumuko wa bei ya huduma na bidhaa,
kuhamasisha usafirishaji na uuzaji wa bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi
kupitia program ya “Export Credit
Guarantee Scheme” na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za
Kigeni.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma
na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa
akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Devotha Mathew
Minja aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kulinda thamani ya Shilingi
kwa kuwa wapo wamiliki wa majengo ambao wanapangisha majengo kwa kutumia fedha
za kigeni kama vile Dola ya Kimarekani badala ya fedha ya Kitanzania hivyo
kusababisha kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji
alisema kuwa matumizi ya fedha za kigeni sambamba na Shilingi ya Tanzania hapa
nchini yanasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 (The Foreign Exchange Act, 1992), Sheria
ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwaka 2006 na Tamko la Serikali la mwaka 2007
kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kulipia bidhaa na huduma katika soko la
ndani.
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa mwezi
Desemba 2017, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb),
alitoa tamko kwa umma kuwa kuanzia Januari Mosi, 2018 bei zote hapa nchini
zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania zikijumuisha kodi ya nyumba za kuishi na
ofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei ya vyombo vya usafiri na
vifaa vya kielektroniki.
“Bei ambazo walengwa wake wakuu ni
watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na
malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni, ambapo zinajumuisha gharama
za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, visa kwa wageni na gharama
za viwanja vya ndege na hoteli, hata
hivyo wageni hao wanapaswa kutambuliwa kwa vitambulisho vyao kama pasi za
kusafiria na nyaraka za usajili kwa Kampuni”. Alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha aliongeza kuwa viwango vya
kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka bei hizo katika sarafu vinatakiwa
kuwekwa wazi na visizidi vile vya soko, vilevile ni benki na maduka ya fedha za
kigeni pekee ndiyo yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha
kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.
Katika maswali ya nyongeza ya Mbunge huyo alitaka
kujua sababu zinazofanya baadhi ya Taasisi kuendelea kupata na kutoa huduma kwa
Dola, pia alihoji Serikali itapitia lini upya Sheria zake ili kuwa na sheria
itakayozuia matumizi ya fedha za Kigeni kama ilivyo kwa nchi ya Afrika Kusini.
Dkt. Kijaji alisema kwa kuwa wajibu
wa marekebisho na kupitisha Sheria ni wa
Bunge hivyo basi, iwapo sheria iliyopo
ina upungufu ni vema kukafanyika maboresho kupitia Bunge.
“Ikumbukwe kuwa katika misingi ya Uchumi mambo
yanayosababisha kushuka au kudorora kwa thamani ya fedha yeyote duniani ni
pamoja na Nakisi ya Urari wa Biashara ambapo kwa Serikali ya Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa katika
kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini” alisema Dkt. Kijaji.
Alibainisha kuwa Mfumuko wa bei na
tofauti ya Msimu huchangia kushuka kwa thamani ya fedha ambapo Tanzania
inaendelea kudhibiti mfumuko huo na Serikali tayari imefunga zaidi ya maduka 92
ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo yameshindwa kufuata sheria na taratibu za
nchi ili kudhibiti maduka hayo kuwa kichaka cha kusafirisha fedha za Tanzania
isivyo halali mambo ambayo yanaonesha juhudi za Serikali kuimarisha kwa kiwango
kikubwa thamani ya shilingi.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
16/4/2018
0 Comments