Subscribe Us

header ads

Atakaethubutu kuvamia tena msitu wa hifadhi uzigua kukiona-Rc Ndikilo

Ofisa msaidizi wa misitu Bagamoyo,Jonathan Mpangala,akionyesha mipaka ambayo imewekwa katika msitu wa hifadhi ya Taifa Uzigua ,wakati mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo (wa katikati mwenye suti)alipotembelea msitu huo .
(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo

MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo ,amekemea wenye nia ya kuvamia msitu wa hifadhi -Uzigua wilayani Bagamoyo na atakaethubutu kufanya hivyo tena atakiona.

Aidha ,ameutaka wakala wa misitu kanda ya Mashariki na wilayani hapo ,kuendelea kukaza uzi katika kufanya doria mbalimbali ili kudhibiti uvamizi uliokuwepo kipindi cha nyuma .

Akizungumza wakati alipokwenda kutembelea msitu wa Uzigua ,kujiridhisha kama umeanza kurejesha uoto wake wa asili ,Ndikilo aliwaasa wananchi wakiwemo wafugaji kuheshimu mipaka iliyopo na kuulinda msitu huo.

Alieleza kuwa ,mwaka mmoja uliopita serikali ilifanya operesheni kali ambapo waliondoa kaya zaidi ya 500 na maboma ya mifugo ya ng'ombe.

Hata hivyo Ndikilo alisema ,kwasasa kumewekwa vigingi vidogo na vikubwa kama mipaka vinaoonyesha upande wa msitu na upande wa wananchi hivyo wasiendelee kuingilia mapito ya njia zinazopita msituni humo na msitu wenyewe.

"Kuna watu walivamia na wengine kuanza kuishi, kuvuna mbao, kukata miti kwa ajili ya mkaa, kuni ,kufuga ng'ombe, kilimo, uchimbaji wa madini,na kusababisha athari kubwa kwa msitu " 

"Msitu huu ni eneo la maji yanayoingia mto Wami, tuliondoa watu wote ,na leo nimepita nimejiridhisha ,nimeona wanyama wameanza kurejea, wanyama wana njia zao hususan tembo ,tumeona wameanza kupita kwenye mapito yao kuelekea Wamimbiki,Saadan,;"
"Miti imeanza kuota ,hivyo uoto wa asili unajirudia kama zamani, hivyo jamii ikiiona inafukuzwa katika misitu ijue misitu ina manufaa kwao " alisema Ndikilo.

Mkuu huyo wa mkoa alichukua fursa hiyo kuiomba jamii iheshimu na kuilinda misitu ya Uzigua ,Kazimzumbwi -Kisarawe,Ruvu Kusini na Wamimbiki ambao wanapakana na Morogoro.

Nae mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ,alhaj Majid Mwanga,alisema tatizo lililopo ni muingiliano wa mifugo hali inayosababisha wakulima kujiona kama wanabaguliwa .

Alielezea ,tayari wamekaa katika vikao vyao wameomba fedha kwa ajili ya kuondoa wafugaji watakaokaidi .

Alhaj Mwanga alisema, iifikie hatua jamii ikawa na uelewa wa makusudio ya serikali yao na kuachana na tabia ya kutaka kuhalalisha mambo yasiyokuwepo.

Ofisa msaidizi wa misitu Bagamoyo,Jonathan Mpangala,alisema msitu huo ulitangazwa na serikali kwa tangazo namba 466 ,la mwaka 1958.

Alisema kuna wilaya tatu zilizoingilia msitu huo ikiwemo vijiji nane vya wilaya ya Bagamoyo,vijiji viwili wilaya ya Kilindi na Handeni ni kijiji kimoja .

Mpangala alisema wakala wa misitu ulipoanza mwaka 2014 ndipo msitu wa Uzigua ulipimwa tena rasmi ,ukiwa na ukubwa wa hekta 24,436 ama kwa tafsiri ya hekari 61,090 ambako katika kipindi hicho walitoa tangazo la kuwataka wavamizi waondoke.

Kwa mujibu wa Caroline Marundo kutoka TFS Kanda ya Mashariki, alimhakikishia mkuu wa mkoa ,kuwa msitu upo shwari .

Alisema hali inaridhisha kwani hakuna usumbufu wa watu kufanya shughuli zozote za kijamii.

Post a Comment

0 Comments