NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
25 MAY 2018
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri
amewaagiza Waganga Wakuu wa Wilaya (DMO) na Maofisa Ushirika kushirikiana na
viongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya ili kuhakikisha kuwa wanachama wote wa Vyama vya Ushirika vya
Msingi(AMCOS) wanajiunga na Ushirika Afya ili waweze kuwa na afya nzuri wakati
wote.
Hatua itawafanya kuwa na mazingira
mazuri ya kupata matibabu ya aina yoyote hapa nchini jambo linalowafanya kuwa
na uhakika wa uzalishaji mazao kwa wingi bila kuwa na kikwazo cha kupata tiba
wakati wakiendelea na shughuli zao.
Mwanri alisema hayo jana wakati
akiwa katika ziara yake kwenye Wilaya ya Igunga ya kuhamasisha wakulima wa
pamba kujiunga na Bima ya Ushirika Afya na pia kupambana na utoro na mimba za
utotoni.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka
Watendaji hao kuhakikisha wanakuwepo katika masoko yote ya mazao ya biashara
ili kutoa elimu na hatimaye kuwasaidia kuwasajili wanachama wa AMCOS ambao
watapenda kujiunga na Bima hiyo.
Alisema ni vema wananchi wajue kuwa mfumo
wa Bima hiyo utamwezesha kutibiwa popote hapa nchini na kuondokana na matumizi
ya fedha nyingi kutokana na kulipa fedha tasimu.
Mwanri alisema mtindo wa kisasa wa
kuishi popote duniani ni kujiunga na Bima ya Afya kwa kuwa inasaidia kupunguza
makali ya matumizi ya fedha kwa ajili ya
matibabu ya aina mbalimbali ambayo huzuka bila hodi wala kuja kuwa wakati
yanakuja una fedha.
Kwa upande wa Meneja wa Mkoa wa
Tabora wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Vedastus Kalungwani alisema kwa
gharama ya shilingi 76,800/- mwanachama atapata matibabu ya aina yoyote katika
vituo vya afya 6,000 nchini kote.
Alisema Bima hiyo itamwezesha
mwanachama kupata matibabu kuanzia Zahanati hadi Hospitali ya Taifa kwa gharama
hizo.
Naye Mwenyekiti wa Chaama Kikuu cha
Ushirika cha Ingembensabo Lazaro Ngullo alisema kuwa huduma ya tiba anayopatiwa
mwanachama wa Bima ya Afya ya aina yoyote inampa unafuu kuliko kama angetumia
fedha tasilimu kupata matibabu ya aina ile ile.
Alisema Bima ya Afya inapunguza
machungu ya gharama ambazo ungezitumia kama ungetoa fedha tasilimu na kuongeza
kuwa ni vema wanaushirika wakachangamkia Bima ya Ushirika ili waweze kufaidi
matunda ya jasho lao.
Ngullo alisema matatizo ya ugonjwa
hayana hodi yanaweza kuzuka wakati wowote uwe na feda au hauna na hivyo ili
kukabiliana nayo ni vema wanaushirika wakakata Bima ili kujiweka tayari wakati
wowote.


0 Comments