Subscribe Us

header ads

Hotuba ya naibu waziri wa afya Dk. Faustine Ngugulile katika uzinduzi wa AMREF hearth africa tanzania

 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisema jambo mbele ya Wakurugenzi na Wawakilishi kutoka taasisi zisizo za Kiserikali katika siku ya uzinduzi wa mradi wa Amref Health Africa wa kupambana na ukimwi na kifua kikuu unaofadhiliwa na mfuko wa dunia (Global Fund).
 Mkurugenzi Mkazi wa amref health afrika Tanzania Dkt. Florence Temu akisoma hotuba mbele ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa mradi wa Amref Health Africa wa kupambana na ukimwi na kifua kikuu unaofadhiliwa na mfuko wa dunia (Global Fund).
 Mkurugenzi Mtendaji wa TAYOA Peter Masika akitoa neon la shukrani mbele ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile, Wakurugenzi na Wawakilishi wa taasisi zisizo za Kiserikali wakati wa uzinduzi wa mradi wa Amref Health Africa wa kupambana na ukimwi na kifua kikuu.
  Wakurugenzi na Wawakilishi wa taasisi zisizo za Kiserikali wakifuatilia kwa makini tamko la Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa mradi wa Amref Health Africa wa kupambana na ukimwi na kifua kikuu unaofadhiliwa na mfuko wa dunia (Global Fund).

 Mwakilishi kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa akibadilishana mkataba wa makubaliano na Mkurugenzi Mkazi wa amref health afrika Tanzania Dkt. Florence Temu baada ya kusainiwa na pande zote mbili wakati wa uzinduzi wa mradi wa Amref Health Africa wa kupambana na ukimwi na kifua kikuu unaofadhiliwa na mfuko wa dunia.
 Mkurugenzi Mtendaji wa TAYOA Peter Masika akibadilishana mkataba wa makubaliano na Mkurugenzi Mkazi wa amref health afrika Tanzania Dkt. Florence Temu baada ya kusainiwa na pande zote mbili wakati wa uzinduzi wa mradi wa Amref Health Africa wa kupambana na ukimwi na kifua kikuu unaofadhiliwa na mfuko wa dunia.
Picha ya pamoja ikiongozwa na mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile na Mkurugenzi Mkazi wa amref health afrika Tanzania Dkt. Florence Temu wakiwa na Wawakilishi wa taasisi zisizo za Kiserikali wakati wa uzinduzi wa mradi wa Amref Health Afrika wa kupambana na ukimwi na kifua kikuu unaofadhiliwa na mfuko wa dunia.
…………………………………………………
Napenda kutumia fursa hii kulishukuru shirika la Amref Health Africa Tanzania  kwa  kunialika kuja kushiriki katika uzinduzi wa Mradi huu wa kupambana na UKIMWI na Kifua Kikuu unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia (Global Fund). 
Miradi inayofadhiliwa na  Mfuko huu wa Dunia imekuwa Tanzania kwa muda mrefu sasa na imekuwa ikitoa mchango muhimu sana katika sekta ya afya hususani katika kupambana na magonjwa matatu ambayo ni  (UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria).
Ndugu wageni waalikwa, kwa namna ya pekee kabisa naomba kuipongeza Amref Health Africa  chini ya uongozi wake Dkt. Florence Temu   kwa kuwa  mstari wa mbele  katika kuboresha sekta ya afya kupitia miradi mbalimbali ya afya hapa nchini. Hivi karibuni Amref Health Afrika ilikuwa inasherehekea miaka 60 ya uwepo na utekelezaji  wa miradi yake hapa barani Africa. 
Binafsi nawapongeza sana  kwani limekuwa ni shirika kongwe lenye kujali maendeleo ya sekta ya  afya kwa Manufaa ya wanajamii wote.
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana, Mradi  huu wa UKIMWI na Kifua Kikuu ni Mradi unaofadhiliwa na mfuko wa Dunia (The Global Fund) na utatekelezwa  na Amref Health Africa kama mpokeaji mkuu kwa upande wa sekta binafsi (Private Sector Principal Recipient) baada ya Wizara ya Fedha ambayo ni mpokeaji mkuu upande wa serikali (Public Sector Principal Recipient) wa fedha za mfuko wa dunia. 
Nimefahamishwa kuwa katika kutekeleza mradi huu Amref Health Africa itafanya kazi kwa ushirikiano na mashirika mengine manne ambayo ni Management Development for Health (MDH), Tanzania Youth Alliance (TAYOA), Tanzania Health Promotion Support (THPS) na Benjamini Mkapa Foundation (BMF).
Ndugu wageni waalikwa, Dhamana hii  tuliyopewa na  mfuko wa dunia ni kubwa sana kama nchi na vilevile  mashirika husika yameaminiwa  katika weledi wa  kutekeleza mradi huu.
 Siku ya leo tunapokuwa hapa na kushuhudia uzinduzi wa mradi huu, basi ni  ishara kuwa  saini au makubaliano yatakayofikiwa katika pande zote yakatekelezwe kwa  umahiri , uwazi, usanifu na uaminifu wa hali ya juu. 
 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaahidi kuendelea kutoa   ushirikiano na muongozo stahiki    ili  kuhakikisha malengo na dhamira ya mradi huu  inafikiwa kwa wakati.
Wizara ya Afya inaendelea kuweka msisitizo wa kutekeleza kwa kufuata taratibu, sheria na miongozo mbalimbali iliyowekwa kitaifa. 
Serikali kwa kushirikiana na wadau tumefanikiwa kutengeneza na kuweka miongozo mbalimbali ili kuhakikisha ufanisi na utaratibu mzuri unafuatwa katika kutekeleza mipango iliyoainishwa. 
Hii itasaidia  kuepuka utendaji usio  sahihi au  kila mtu kutekeleza kwa namna yake na mwisho wa siku kuharibu ubora wa malengo yaliyotarajiwa.
Ni mwezi huu tu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tulizindua Mpango Mkakati wa Nne wa Kudhibiti Ukimwi katika Sekta ya Afya (National HSHSP IV 2017-2022).
 Mkakati huu utasaidia kuweka mazingira wezeshi katika kutekeleza mradi huu husasani afua zinazolenga UKIMWI.  
Kukumbushia vitu vichache katika mpango huo Serikali ya Tanzania inakusudia kufikia mwaka 2022 asilimia 95% ya watu wote wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kuwa kwenye dawa. 
Vile vile, kuhakikisha ifikapo 2022 asilimia 90% watoto waliofikia vigezo na wanaoishi na maambukizi wanabaki kwenye dawa na 95% ya watu wazima wanapatiwa ART na kuendelea kubaki kwenye dawa.
Kwa upande wa Kifua Kikuu tunao Mpango Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma wa mwaka 2015-2020. Vile vile utekelezaji wa mpango wa kidunia wa kutokomeza Kifua Kikuu,  na  Kuchangia katika malengo ya maendeleo endelevu katika kutokomeza janga la ugonjwa wa kifua kikuu au TB ifikapo mwaka 2030.
  Kifua kikuu (TB) bado ni tatizo nchini kwetu. Jumla ya Watu 160,000 wanakadiriwa kuwa na ugonjwa huu nchini Tanzania.
 Jumla ya Wagonjwa wapya wapatao 68,819 waliibuliwa  mwaka 2017 ikilinganishwa na 62,182 mwaka 2015. 
Mkakati wa shirika la afya ulimwenguni, WHO wa kutokomeza TB unataka kupungua kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa asilimia 90.
 Malengo yote haya yatafikiwa iwapo tutafanya kazi kwa   umakini na ushirikiano kati ya wadau wote.
Ndugu wageni waalikwa, sambamba na utekelezaji wa mradi huu, serikali imeweka mfumo mzuri ili kuhakikisha taarifa zinakusanywa na kuripotiwa kwa wakati. 
 Tunatambua kumekuwa na changamoto ya upatikanaji  wa taarifa kwa kuipitia mfumo wa taarifa wa afya wa Wilaya DHIS2 lakini kwa sasa hali imeboreka.
 Kupitia Program za Wizara (NACP and NTLP) na kwa kushirikiana na wadau  wengine taarifa zimekuwa zinaboreshwa na kupatikana kwa urahisi.
 Tuendelee kuhimiza katika hili, kwani  kama tutafanya kazi nzuri  lakini  taarifa zake hazipatikani kwa urahisi na  kwa wakati haitatusaidia katika kufanya maamuzi  mbalimbali muhimu kwa jamii na kwa taifa kwa ujumla.
Ndugu watanzania wenzangu, Naomba kusisitiza kwa mara nyingine, unapopewa dhamana ya kuongoza au kutekeleza mradi wenye kunufaisha afya ya mamilioni ya  watanzania , basi onyesha weledi wako maradufu.
 Hicho kitakuwa kigezo  tosha cha kuendelea kuaminiwa na  kupata sifa stahiki popote duniani.
 Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kushirikiana kwa karibu sana ili kuhakikisha kua mradi huu unakamilika kwa wakati na kuwafikia  walengwa.
Nawashukuruni sana kwa kunisikiliza, , naomba sote tusimame kwa pamoja kushuhudia  Mradi huu wa Global Fund wa Ukimwi na Kifua Kikuu UKIZINDULIWA Rasmi.

Post a Comment

0 Comments